MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya soka Bara, Yanga
wameshindwa kutamba ugenini kwenye Uwanja wa Namfua Singida dhidi ya Singida
United baada ya kulazimishwa suluhu.
Yanga iliyokuwa na pointi 16 sasa imefikisha pointi 17 huku
Singida United ikifikisha pointi 14 kwenye msimamo wa ligi ambao ulitarajiwa
kubadilika baada ya matokeo ya Azam na Ruvu Shooting zilizotarajiwa kuchezwa usiku.
Wenyeji Singida United walitawala mpira kipindi cha kwanza
na cha pili na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga ingawa ilishindwa kuzitumia
kwa vipindi tofauti.
Safu ya kiungo ya Singida ilifanya vizuri kwa kutengeneza
nafasi na mashambulizi ila washambuliaji walishindwa kufunga.
Upande wa Yanga, nafasi ya kiungo ilizidiwa na kushindwa
kutengeneza nafasi za kufunga.
Kipindi cha kwanza kilimalizika Singida ikiongoza kwa
mashambulizi mengi na hata kipindi cha pili bado walikuwa bora zaidi ya Yanga
walioonekana kuzidiwa karibu muda mwingi.
Tafwadzwa Kutinyu alipata nafasi ya kufunga katika dakika
ya 17 na 43 na kushindwa kutumia baada
ya kipa wa Yanga, Youthe Rostand kuzipangua. Pia, Deus Kaseke na Danny
Usengimana walikuwa wakipata nafasi na kushindwa kuzitumia.
Kwa upande wa Yanga, Geofrey Mwashiuya alipata nafasi
akashindwa kuitumia.
Timu zote mbili zilifanya mabadiliko Singida ilimtoa Kaseke
na kuingia Nhivi Simbarashe, Usengimana alitoka na kuingia Atupele Green, Yanga
iliwatoa Mwashiuya na kuingia Emmanuel Martin na Raphael Daud aliingia kuchukua
nafasi ya Pato Ngonyani lakini bado hakuna timu iliyopata ushindi.
Mechi nyingine zilizochezwa jana ni Mtibwa Sugar dhidi ya
Ndanda zilizotoka suluhu matokeo kama hayo yalipatikana katika mechi ya Njombe
Mji dhidi ya Mbao huku Kagera Sugar ikitoka sare ya bao 1-1 na Tanzania
Prisons.
No comments:
Post a Comment