BASATA YAWAPA MC NA MA-DJ MUDA WA MWISHO KUJISAJILI
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limetoa agizo rasmi kwa Waongoza Sherehe, Burudani na Matukio (MC) pamoja na Manju wa Muziki (DJ) nchini kote kuhakikisha wanasajiliwa na kuwa na vibali hai vya kufanyia kazi ifikapo tarehe 31 Januari, 2026.
Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa Kanuni ya 18 na Kanuni ya 20 ya Kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa za mwaka 2018, zikisomwa pamoja na Jedwali la Pili la Tozo za BASATA za Mwaka 2025.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa BASATA, Bw. Leonidas Tibanga, imefafanua kuwa kuwa na kibali hai ndiyo kigezo pekee kitakachompa mdau uhalali wa kisheria wa kufanya shughuli hizo za sanaa.
Katika kurahisisha zoezi hili, BASATA imeweka wazi kuwa gharama za usajili ni shilingi elfu kumi (10,000/=) na ada ya kibali ni shilingi elfu arobaini (40,000/=), ambapo wadau wanatakiwa kujisajili kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya sanaa.go.tz.
Aidha, Baraza limetoa onyo kali kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayepatikana anafanya kazi kinyume na utaratibu huu baada ya muda uliopangwa kupita.

Post a Comment