TIMU ya wasichana ya Tanzania imekabidhiwa zawadi ya Sh milioni 16 baada
ya kutwaa ubingwa wa michuano ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17 ya
Kimataifa ya Airtel Rising Stars iliyofanyika Septemba mwaka jana nchini
Nigeria.
Timu hiyo ilitwaa taji hilo baada ya kuifunga Kenya bao 1-0 lililofungwa
na Donisia Daniel katika fainali hizo.
Akipokea fedha hizo jana Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar
es Salaam (DRFA), Msanifu Kondo alisema wanaishukuru Kampuni ya Airtel kwa
kutimiza ahadi yao na wamezikabidhi kwa makocha na wachezaji wa timu hiyo.
Alisema kila mchezaji amepewa Sh 850,000 wakati kocha mkuu wa timu hiyo
Rogasian Kaijage amepewa Sh milioni moja na laki mbili na kocha msaidizi
amepewa Sh milioni moja.
“Tunawashukuru Airtel kwa kutoa
fedha hizo za zawadi kwa timu hii na sisi tumewakabidhi wahusika,” alisema.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa Airtel Tanzania Jane Matinde alisema
wao kama wadhamini wa mashindano hayo wametimiza ahadi yao kwa kukabidhi fedha
hizo kwa mabingwa hao.
“Kwa niaba ya Airtel Tanzania tunaipongeza timu ya wasichana ya Tanzania
kwa kutwaa ubingwa huo, lakini pia tumetekeleza ahadi yetu ya kukabidhi zawadi,
kama mnavyofahamu kampuni yetu imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia mambo ya
kijamii lakini pia michezo ikiwemo soka kupitia michuano ya vijana ya Airtel
Rising Stars kwa kushiriki na klabu ya Manchester United,” alisema.
No comments:
Post a Comment