Kocha na mzee Said wakiwasili kwenye chumba cha mkutano kuzungumza na waandishi wa habari
KOCHA Joseph Omog amesaini
mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha klabu ya Azam kwa ajili ya mzunguko wa
pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa mwakani.
Omog raia wa Cameroon, amewasili nchini leo na moja kwa moja akasaini
mkataba wa miaka miwili wa kuwafundisha wawakilishi hao wa Tanzania kwenye
mashindano ya kombe la Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), akichukua mikoba
iliyoachwa na Stewart Hall.
Hall alitangaza kujiuzulu
kuifundisha timu hiyo baada ya mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania
Bara dhidi ya Mbeya City, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Chamazi na
kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.
“Tumepitia historia na
uzoefu wake tukaone tumpe jukumu la kuifundisha timu yetu kwa kipindi cha miaka
miwili,” alisema Mwenyekiti wa Klabu ya Azam, Said Mohamedi
“Historia yake inaonesha
kuwa ana uzoefu mkubwa kwenye mashindano ya kimataifa, kwani aliwahi kuiwezesha
Leopards ya Congo Brazaville kutwa kombe la Shirikisho la Soka la Afrika (CAF),
mashindano ambayo timu yetu itashiriki.
Mohamedi alikataa kuweka
wazi kiwango cha fedha atakacholipwa kocha huyo kwa hoja ya kwamba hiyo ni siri
baina ya klabu hiyo na kocha huyo.
Akizungumza kwenye
utambulisho huo, Omog alisema kuwa ana furaha kupewa jukumu la kuifundisha Azam
na kusema kuwa ni timu anayoifahamu kwani aliiona wakati ikishiriki mashindano
ya Kombe la CAF mwaka jana.
“Jukumu langu ni kuona kuwa
timu hii inafanya vizuri kwenye ligi na pia kwenye mashindano ya Kombe la CAF,
lakini hilo litawezekana kutokana na ushirikiano kutoka kwa wachezaji na
viongozi wa timu hii,” alisema Omog aliyekuwa akizungumza kwa lugha ya
kifaransa na mwanae Henry Omog ambaye ndiye Meneja wake kutafsiri kwa lugha la
Kiingereza.
|
No comments:
Post a Comment