Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, August 11, 2013

SIMBA ILIVYONOGESHA TAMASHA LAO KWA KUIFUNGA SPORTS CLUB VILLA 4-1

Haroun Chanongo akijaribu kumtoka beki wa SC Villa ya Uganda


Amri Kiemba akijaribu kumtoka nahodha wa SC Villa jana





MAADHIMISHO ya tamasha la Simba Day, linalofanyika kila mwaka, jana yalinogeshwa na vionjo mbalimbali, ukiwemo ushindi wa mabao 4-1 ambao timu hiyo iliupata dhidi ya SC Villa ya Uganda na utambulisho wa mshambuliaji Mrisho Ngassa.

Simba iliialika SC Villa kwa ajili ya kunogesha sherehe hizo, ambazo zinafanyika kwa mwaka wa tano sasa.
Kivutio zaidi katika tamasha hilo ni ushindi wa mabao 4-1 ambao Wekundu hao waliupata, ambao uliongeza burudani na kukonga nyoyo za mashabiki wa timu hiyo.
Mechi ilianza huku timu zote mbili zikionekana kukamiana na kushambuliana kwa zamu na walikuwa SC Villa walioanza kupata bao kunako dakika ya 9 tu ya mchezo, kupitia kwa Mganga Robert, ambaye alimalizia pasi ya Sijali Jamal.

Simba haikuchanganyikiwa na bao hilo na badala yake ilitulia na kuongeza mashambulizi zaidi, huku ikisaka bao la kusawazisha ambalo walifanikiwa kulipata dakika ya 43, kupitia kwa Jonas Mkude, kwa shuti la umbali wa mita 18, lililojaa moja kwa moja wavuni na kuyafanya matokeo kuwa 1-1 hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.

Kipindi cha pili kilipoanza, iliwachukua Simba dakika nane tu kuandika bao la pili, kupitia kwa  William Lucian, ambaye naye alipiga shuti kali la umbali wa mita 18 lililojaa wavuni, akiunganisha krosi ya Issa Rashid 'Baba Ubaya.'
Shujaa wa mchezo huo alikuwa ni Betram Mombeki, ambaye alifunga mabao mawili dakika za 70 na 72, kuifanya Simba kuondoka uwanjani na ushindi wa mabao hayo 4-1.

La kwanza alilifunga kwa shuti kali la mbali, huku la pili likitokana na krosi ya Said Ndemla.
Simba baadaye ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Mombeki na nafasi yake kuchukuliwa na Ramadhani Singano 'Messi', akaingia Hassan Hatib badala ya Joseph Owino na Marcel Kaheza akamrithi Haroun Chanongo.
Mashabiki wa Simba waliohudhuria uwanjani kushuhudia mechi hiyo walionekana wenye furaha kubwa baada ya kuikosa kwa muda mrefu.

Awali kikosi cha Simba B, kilichezea kichapo cha mabao 6-3 kutoka kwa timu ya vijana ya Twalipo.
Tukio kubwa lililojiri uwanjani humo jana ni kitendo cha Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, kumtambulisha Mrisho Ngassa, kuwa miongoni mwa wachezaji waliotambulishwa kuwemo kwenye kikosi cha timu hiyo cha msimu huu, licha ya kudaiwa kutimkia Yanga na kutokuwepo uwanjani.

Kikosi cha Simba kilichoanza kilikuwa: Abel Dhaira, Masoud Nassoro 'Chollo', Issa Rashid Baba Ubaya' Joseph Owino, Miraji Adam, Jonathan Mkude, Ramadhan Chombo 'Redondo', Abdulhalim Humud, Betram Mombeki, Amri Kiemba na Haroun Chanongo.

No comments:

Post a Comment