WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema uzinduzi wa vifaa vya kisasa
vya kurushia matangazo ya mpira wa miguu na video za usaidizi wa waamuzi (VAR)
vitasaidia kuleta mashindano mengi ya kimataifa nchini.
Aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa vifaa hivyo vya Azam Media
uliofanyika katika Uwanja wa Benjamini Mkapa jana.
“Azam Media mmetupeleka kwenye vigezo vya Afcon kuchezwa Tanzania,
kutokana na ubora wa vifaa vyenu na huu uzinduzi wa VAR,” alisema Majaliwa.
Alisema VAR itasaidia kuondoa malalamiko kwa timu pamoja na
kupunguza makosa ya kibinadamu kwa waamuzi na kuwa makini katika kazi zao.
Vilevile alisema soka la Tanzania limeendelea kukua kwa sababu ya
maboresho ya miundombinu kwa sekta zote ikiwemo Azam Media kwa kuleta mitambo
imara ambayo itawezesha soka letu kuonekana sehemu mbalimbali nchini na nje ya
nchi.
“Kazi iliyopo TFF ni kuwapa masharti wamiliki wa viwanja,
asiyetimiza awekwe pembeni. Tunahitaji kufika mbali kwenye viwango vya Afrika
baada ya namba sita basi tuwe namba nne au mbili, ili tukapambane na Morocco na
Misri,” alisema Majaliwa.
Vilevile alisema serikali itatimiza ahadi ya waziri aliyepita
katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa juu ya kuleta
VAR kama ilivyoahidiwa.
Aidha, alisema serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeingia
kwenye sekta ya michezo na kutoa hamasa mbalimbali kwenye michezo ikiwemo goli
la mama ambalo limeongeza hamasa kwa timu kufanya viuri kwenye michuano ya
kimataifa.
“Rais amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha kwa kutoa goli la mama
kwa timu za taifa hata klabu ambazo zitashiriki michuano ya kimataifa,” alisema
Majaliwa.
Vilevile alisema Tanzania kuwa mwenyeji michuano ya Afcon 2027 ni
jitihada za Rais Samia kwa ushirikiano na wenzake wa Kenya na Uganda, William
Ruto na Yoweri Museveni.
No comments:
Post a Comment