SIMBA leo imejikita kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara baada
ya kuifunga Singida United kwa mabao 4-0 katika mchezo uliofanyika kwenye
Uwanja wa Taifa.
Simba
ilianza kuandika bao katika dakika ya tatu ya mchezo baada ya
Shizza Kichuya kufunga baada ya kutuliza mpira na kuujaza wavuni kwa juu.
Dakika nne
baadae, Nicolas Gyan nusura afunge, lakini akiwa katika nafasi nzuri,alipiga
mpira nje.
Asante Kwasi
akiichezea Simba kwa mara ya kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu tangu ajiunge
nayo katika dirisha dogo la usajili akitokea Lipuli ya Iringa, alifunga katika
dakika ya 24.
Wachezaji wa
Singida walifikiri mfungaji atakuwa ameotea na kusita kumzuia na kupatikana kwa
bao hilo.
Dakika ya 76,
Emmanuel Okwi aliyeingia kipindi cha pili, aliifungia Simba bao la tatu na
kuifanya timu hiyo kuzidi kuwa na uhakika wa kutoka na pointi zote tatu.
Okwi ambaye alirejea juzi kutoka kwao Uganda, ambako
alikaa zaidi ya muda alioruhusiwa, alifunga bao la nne baada ya kupata pasi
kutoka kwa Ndemla baada ya kumkwepa kipa.
Kwa ushindi
huo, Simba sasa imefikisha pointi 29 baada ya michezo 13 na kuiacha Azam FC ya
pili na pointi zake 27 huku Yanga ikibaki katika nafasi ya tano kwa pointi zake
22.
Azam ambayo imekalia kwa muda kiti cha uongozi wa ligi baada ya kutoka sare ya 1-1 na
Majimaji ya Songea katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Majimaji, huku
Yanga jana ikilazimishwa suluhu na Mwadui ya Shinyanga kwenye Uwanja wa Taifa.
Ushindi huo
ulishuhudiwa na kocha mpya wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre aliyekuwa
jukwaani wakati timu hiyo ikitoa kipigo hicho.
Kwa mujibu
wa taarifa ya Simba, klabu hiyo wakati wowote itaingia mkataba na kocha huyo
aliyeipatia Cameroon ubingwa wa Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2000.
Vikosi vilikuwa, Simba: Aishi Manula, Nicholas Gyan, Asante
Kwasi, Juuko Murdhid, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, James Kotei/Mohamed Ibrahim,
Mwinyi Kazimoto, John Bocco, Shiza Kichuya na Mzamiru Yassin/Emmanuel Okwi.
Singida: Peter Manyika, Micahel
Rusheshagonga, Shafik Batambuzi, Kenned Wilson, Maliki Antiri, Mudathir Yahya,
Deus Kaseke, Tafwadza Kutinyu/Yusuph Kagoma, Lubinda Mundia/Kenny Ally, Kambale
Salita na Kiggi Makasi/Elinywesia Sumbi.
No comments:
Post a Comment