*Mabao yaliyofungwa na klabu na walioruhusu mengi
*Pia Makocha waliopoteza kazi, idadi
ya watazamaji
HALI ya leo ya Ligi Kuu ya England (EPL)
ni tofauti sana na mambo yalivyokuwa ilipoanzishwa miaka 25 iliyopita,
zikiwamo klabu ambazo leo kuna baadhi wala hawajapata kuzisikia
kama Oldham Athletic na Wimbledon.
Baada ya mechi 9,746, mabao 25,769 miongoni
mwa timu tofauti 47 zilizokuwa zikipanda na kushuka
lakini kila msimu mmoja zikiwamo 20 tu, kwa hakika kuna kumbukumbu nzuri
katika miaka 25 ya ligi hii tangu ilipoanzishwa 1992.
Hii ni ligi ambayo imekuwa ikionwa
kama mahali pasipo salama kwa makocha wengi, labda mmoja tu Arsene
Wenger wa Arsenal ambaye amekuwa akihakikishiwa usalama wake na
kwamba angeweza kukaa muda wote hadi anapoamua kuondoka; na
bado yupo.
Msimu wenyewe wa ufunguzi haukuacha
mtu salama, kwani Chelsea walimfukuza kocha wao Ian
Porterfield aliyepoteza mechi 29 kati ya 42 zilizokuwa mikononi mwake. Februari
15, 1993 haitakaa iwe siku nzuri kwake kwani ndipo alipofunguliwa
mlango na kusukumwa nje ya Stamford Bridge.
Kati ya Agosti 1994 na 1995 mambo yaliendelea,
ambapo jumla ya makocha 15 waliondoshwa kwenye nafasi zao kimabadiliko,
kati ya hao wanane wakiwa wamefukuzwa kazi. Awali timu shiriki
zilikuwa 22, lakini zilipokuja fedha za dili za televisheni,
liamuliwa kwamba kila timu icheze mechi 38, hivyo ikabidi timu zipunguzwe
hadi 20, na ndizo zipo hadi sasa.
Wahanga wa panga pangua na fukuza ya
ukocha iliwahusu akina John Deehan aliyeachia ngazi baada ya
jahazi la Norwich kuelekea kuzama wakati Alan Smith alikimbia pale Crystal
Palace waliposhuka daraja.
Kwa waliokuwa wakifuatilia hata
majuzi hapa wanajua kwamba Roberto Mancini alifukuzwa kazi na
Manchester City Mei 2013 – mwaka mmoja tu baada ya kuwapa ubingwa wakati
Claudio Ranieri ‘the Tinkerman’ alipoteza kibarua chake miezi tisa
tu tangu awape Leicester ubingwa wa kwanza tangu kuzaliwa kwao, na
ubingwa wenyewe ulikuja msimu wa 2015/16.
Chelsea walikosa uvumilivu zaidi kwa
sababu Desemba 2015 tu walimfukuza kocha wao, Jose Mourinho
ambaye miezi saba kabla alikuwa amewapa ubingwa lakini sasa alikuwa akiwaelekeza
timu kwenye kushuka daraja. Hadi kufikia mwisho wa msimu
wa 2016/17 wastani wa mabadiliko ya makocha kwenye klabu za EPL
ulikuwa 8.84.
Idadi hiyo inaelekea itakuwa kubwa zaidi.
Ni katika misimu miwili tu kati ya 10 iliyopita idadi hiyo
imekuwa kwenye tarakimu moja. Kwa ujumla wake katika kipindi hiki cha robo
karne ya EPL pamekuwapo makocha 154 waliohudumu katika namna
ya kudumu huku kukiwapo 67 wa muda, ikimaanisha kocha mkuu
alifukuzwa au kutokuwa kazini kwa sababu yoyote ndipo akakaimiwa.
Katika kipindi hiki cha miaka 25 pamekuwapo
jumla ya wachezaji 3,835 waliocheza walau mechi moja ya EPL.
Rekodi nyingine iliyowekwa ni kwa mshambuliaji
wa zamani wa Everton, Duncan Ferguson ndiye mchezaji aliyepewa
kadi nyingi zaidi nyekundu, akiwa nazo nane katika mechi 269,
ikimaanisha ni kadi moja kwa kila mechi 33.62.
Tunaye mchezaji aliyeshinda ubingwa
wa England mara tatu – Patrick Vieira ambaye pia alipewa kadi nane nyekundu
katika mechi 307 alizochezea Arsenal na Manchester
City, wakati Richard Dunne aliyekipiga mechi 431 akiwa na
Everton, Manchester City, Aston Villa na Queens Park Rangers (QPR) naye alitia
fora kwa kulimwa kadi.
Kwa ujumla wake, kadi nyekundu zilitotoka
ni 1,477 katika kipindi cha miaka 25, ambazo ni wastani wa kadi 59.08
kila msimu, wachezaji waliozipewa wakiwa ni 72 misimu ya 1998/99,
2002/03 na 2005/06 zikiwa ni kadi 44 zaidi
ikilinganishwa na zile zilizotolewa kati ya 1993/94.
Liverpool bwana, pengine wakiitwa
bwawa la maini ni sawa, kwa sababu ya kadi nyekundu 54 walizochuma
katika mechi 962, lakini zilikuwa 32 pungufu ya watani wao wa jadi wa Merseyside
ambao ni Everton katika idadi sawa ya mechi. Sunderland na
QPR walikuwa na idadi sawa ya wachezaji – tisa, waliopewa kadi nyekundu
na pia wakaenda sawa kuepuka kushuka daraja misimu ya 2009/10 na 2011/12
mtawalia.
Everton wanashikilia rekodi ya wachezaji
wake kurolewa nje kwa kadi nyekundu kuliko wengine, ambapo
katika robo karne hiyo ni wachezaji 86, lakini Tofees hao wamecheza pia mechi
nyingi ambazo ni 962. Huo ni wastani wa kadi nyekundu moja kwa
kila mechi 11.18. Hull City wamepigwa kadi nyekundu 24 katika
mechi 190 ikimaanisha ni kadi mchezaji mmoja kutolewa nje kwa kila
mechi 7.91.
Kwenye ufungaji wakoje? Hakuna timu iliyofunga mabao mengi kama Manchester United kwene EPL ambapo mabao yao katika robo karne yalifikia 1,856, wakiwazidi kwa
mabao 158 wanaoshika nafasi ya pili ambao ni Arsenal. Hiyo ni asilimia
7.2 ya mabao yote 25,769 yaliyofungwa humo katika historia isiyofutika na inayozidi kurembwa.
Blackpool wao wamefanikiwa kuweka rekodi ya kushushwa daraja wakiwa na mabao mengi zaidi ya kufunga, ambapo msimu wa 2010/11 walicheka na nyavu mara 55 kwenye mechi 38 lakini bado wakashushwa daraja, wakati walilingana kwa mabao hayo na Spurs walioshika nafasi ya tano.
Katika msimu wa kwanza mamabo yaliyofungwa yalikuwa 1,222 –
mchezaji wa Sheffield United, Brian Deane akifunga bao la kwanza kabisa la
EPL, kwa kichwa, dakika tano tu mchezoni
na ilikuwa dhidi ya Mashetani Wekundu.
Ni timu tatu tu zimefanikiwa kufunga mabao zaidi ya 100 kwenye msimu mmoja nazo ni Chelsea
(103 msimu wa 2009/10), Manchester City (102 msimu wa 2013/14) na
Liverpool (101 msimu wa 2013/14).
Kwa upande mwingine wa dimba,
Swindon Town, ni timu pekee katika msimu
wa 1993/94, walikuwa timu pekee
katika kipindi cha miaka 25 kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 100.
Wachezaji saba wamefunga mabao 30 au zaidi katika msimu mmoja kwenye
robo karne hii ya EPL. Hao ni Andy
Cole (34 – 1993/94), Alan Shearer (34 & 31 – 1994/95, 1995/96), Kevin Phillips (30 – 1999/00),
Thierry Henry (30 – 2003/04), Cristiano Ronaldo (31 – 2007/08), Robin van Persie (30 – 2011/12) ana Luis
Suarez
(31 – 2013/14).
Shearer hadi sasa anashikilia rekodi
ya wakati wote kwa kuwa mfungaji bora akiwa na idadi ya mabao 260 aliyopachika akiwa na klabu za Blackburn na Newcastle, huku Wayne Rooney akishika nafasi ya pili na mabao yake 198 aliyopata akiwa na Everton na Manchester United na sasa anataka kufufua mambo baada ya
kurejea
Everton msimu huu miaka 13 tangu alipoondoka.
Vipi kuhusu watazamani? Walijitokeza 12,681 pale uwanja wa Coventry wa Highfield Road Agosti 15 1992 kwenye ufunguzi wa ligi ambapo Sky Blues waliwapiga Middlesbrough 2-1, wakati Arsenal na Chelsea wote walishindwa kupata watazamani 25,000 kwenye wikiendi hiyo hiyo ya kwanza ya ufunguzi wa ligi.
Lakini walikuwa watazamani 3,039 waliojitokeza kumwona Tony Cottee akiwafungia Everton mara mbili
kwenye ushindi wao wa 3-1 dhidi ya Wimbledon katika dimba la Selhurst
Park Januari 26, 1993 – wakiweka rekodi ya watazamaji wachache zaidi
katika historia ya EPL. Pungufu ya watazamani milioni 10 walijitokeza
kwa ajili ya kutazama mechi 462 msimu huo wa 1992/93 ambapo Chelsea walikuwa na wastani wa 19,000 – wachache.
Lakini sasa tukija kwenye msimu wa 2016/17, jumla ya watu milioni 13.6 walitokea kutazama mechi 380, nusu ya klabu zikivuta watazamaji kuanzia 50,000 na zaidi, ambapo
idadi yao kwenye mabao ilikuwa Manchester United (75,290), Arsenal
(59,957), West Ham (56,972), Manchester City (54,019) na
Liverpool (53,016).
Katika miaka 25 iliyopita klabu
kadhaa, ikiwa ni pamoja na Manchester United, Chelsea na Liverpool wamekarabati na kuongeza ukubwa wa viwanja vyao wakati wengine kama Arsenal, Manchester City na Southampton wamejenga vipya.
Leicester
City walihama kutoka Filbert Street kwenda Walkers Stadium – sasa kukiitwa King Power Stadium mwaka 2002. Kwa minajili ya rekodi pia,
kipa John Burridge akiwa na umri wa miaka 43 na siku 162 alichezea Manchester City dhidi ya QPR Mei 14, 1995, na hadi sasa ameshikilia
rekodi ya kuwa mchezaji wmenye umri
mkubwa zaidi katika miaka hiyo 25 ya EPL. Karibu robo nyingine ya EPL.
No comments:
Post a Comment