Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, July 26, 2017

RAYON SPORTS KUCHEZA NA SIMBA, SIKU YA SIMBA DAY
Tarehe 8-8-2017 klabu ya Simba itakuwa inaadhimisha siku yake maalumu ambayo hutumika kama siku ya kukumbuka kuanzishwa kwake zaidi ya miaka 81 iliyopita. Simba SC almaarufu kama wekundu wa msimbazi wanaotanua kucha zao na kauli mbiu thabiti ya NGUVU MOJA, ilianzishwa mwaka 1936.
Timu ya Rayon Sports mabingwa wa ligi kuu nchini Rwanda , wamepewa mwaliko kucheza na Simba katika maadhimisho hayo yanayofanyika kila mwaka ifikapo tarehe 8 mwezi wa nane.
Rayon Sports ni moja kati ya timu bora ukanda wa Afrika mashariki na kati hivyo inatarajiwa kutoa upinzani mzuri na burudani ya kutosha dhidi ya Simba SC katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Taifa sambamba na shughuli zingine tanzu ambazo huhitimisha siku hiyo muhimu kwa wanamsimbazi ikiwemo ; utambulisho wa jezi rasmi za msimu mpya, utambulishaji wa kikosi kipya , kutoa vyeti kwa nguli wa timu hiyo waliyoitumikia kwa mapenzi makubwa , kutoa sera na muongozo wa msimu mpya wa ligi .
Pia ukataji wa keki maalumu ambayo husimama kama kielelezo cha umoja , mshikamano na upendo mkubwa wa wanachama , wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kongwe nchini ikiwa na historia ya pekee ya kuongoza kuchukua kombe la Kagame kwa ukanda wa Afrika mashariki na kati . Simba wamebeba kombe hilo mara sita mfululizo wakifuatiwa na Yanga SC na Gor Mahia kila mmoja akibeba kombe hilo mara tano (5).
Sherehe za mwaka huu zinatabiriwa kukosa morali kutokana na viongozi wandamizi wa klabu hiyo kuwa rumande kwa tuhuma za utakatishaji pesa kesi ambayo bado inarindima vilivyo mahakamani. Viongozi hao ni Raisi wa klabu hiyo Evansi Aveva na makamu wake Nyange Godfrey Kaburu.
Fununu za usajili wa kiungo wa Yanga SC Haruna Niyonzima zinaweza kuwa kivutio kingine katikati ya ombwe la huzuni ya viongozi wao endapo litatimia.
Kwa sasa mabingwa hao wa kombe la ASFC wapo nchini Afrika kusini kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu na mechi ya Ngao ya jamii dhidi ya mahasimu wao wakubwa Yanga hapo August 24,2017 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.