Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, July 26, 2017

WAZIRI MWAKYEMBE ATOA SHUKRANI KWA WADAU MBALIMBALI, KIFO CHA MKEWE LINAH

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe
akizungumza na waandishi wa habari (hawapo katika picha) leo Jijini Dar es Salaam
alipokuwa akitoa neno la shukrani kwa wote walioshiriki katika kumfariji kipindi cha
msiba wa mke wake mpendwa Bi. Linah George Mwakyembe.

Napenda kutumia fursa hii kwanza kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka
zake na pili kutoa shukrani zangu za dhati kwa Watanzania wote kwa upendo na
ushirikiano mkubwa mlionipa mimi na familia yangu katika kuomboleza kifo cha
mke wangu mpendwa Bi.Linah Widmel-George Mwakyembe na baadaye katika mazishi
yake wilayani Kyela.

Familia inapenda kutoa shukrani za pekee kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli; Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu
Hassan; Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, na Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai kwa
mchango wao mkubwa katika kumuuguza marehemu wakati wa uhai wake.

Aidha, familia inawashukuru viongozi hao waandamizi wa nchi pamoja na Kaimu Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma, Naibu Spika, Mhe. Tulia Ackson
Mwansasu, wake wa viongozi, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, viongozi wetu wa
nchi wastaafu, Wabunge, Majaji, Mabalozi wa nchi mbalimbali, Mufti na Sheikh Mkuu
wa Tanzania, Maaskofu wa Kanisa la Kiluteri, Makanisa ya Moravian na makanisa ya
kiroho (Mito ya Baraka, Living Water, Evangelical Brotherhood nk) kwa ushirikiano wao
katika maombolezi na mazishi ya marehemu.

Wana-familia tutakumbuka daima moyo adhimu wa upendo na ushirikiano tulioupata
toka kwa Katibu wa Bunge na maafisa wake, Katibu Mkuu Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo na timu yake mzima ya Wizara, Makatibu Wakuu
wakiongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi, watendaji wakuu wa taasisi, asasi na kampuni
mbalimbali, na wananchi wote kwa ujumla katika kipindi hicho kigumu.

Pia napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru Wana-Kyela wote kwa uvumilivu
waliouonesha kipindi chote cha kumuuguza marehemu na ushirikiano wao wa dhati
katika mazishi yake.
Mwisho lakini si kwa umuhimu, nawashukuru sana madaktari na
wauguzi waliomhudumia marehemu kwa kujituma, kwa weledi na ustahimilivu wao ili
kuokoa maisha yake lakini Mungu akampenda zaidi. Vilevile wamiliki wa vyombo vya
habari, waandishi na watangazaji kwa kukesha nasi kipindi chote cha msiba Dar es

Salaam na Kyela wakitekeleza wajibu wao wa kitaaluma na vilevile kutufariji wafiwa
kwa hali na mali.
Nawaomba wote mpokee shukrani zangu za dhati na Mwenyezi Mungu awabariki kwa
moyo wa ushirikiano na upendo mliouonyesha kwetu.

Bwana alitoa na Bwana Ametwaa, jina lake lihimidiwe.

Dkt. Harrison George Mwakyembe (Mb),

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO,

26/07/2017.