Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, March 1, 2017

YANGA YAIFUNGA RUVU SHOOTING 2-0 UWANJA WA TAIFA

YANGAimerejea kwenye mstari baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ruvu Shooting katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mabingwa hao watetezi wa ligi hiyo, walipata ushindi ikiwa zimepita siku chache baada ya kupoteza mechi dhidi ya watani wa jadi, Simba kwa kufungwa mabao 2-1.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 52 ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Simba yenye pointi 54 kileleni, zote zikiwa zimecheza mechi 24 na kuzidi kunogesha mbio za ubingwa kutokana na kupishana pointi chache.
Simon Msuva ndiye aliyeanza kupeleka shangwe Jangwani jana baada ya kufunga bao la mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi Ahmed Simba wa Kagera katika dakika ya 32.
Hata hivyo, Yanga ililazimika kwenda mapumziko pungufu baada ya mchezaji wake Obrey Chirwa kutolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 45 baada ya kuudunda mpira chini kufuatia faulo aliyofanya mwenyewe, awali alikuwa na kadi ya njano kwa kushika mpira.
Bao la pili la Yanga lilifungwa na Emmanuel Martin katika dakika ya 90 akiunganisha krosi ya mpira wa kichwa iliyochongwa na Msuva na kuujaza mpira wavuni.
Kwa ujumla Yanga ilitawala sehemu kubwa ya mechi hiyo ambapo kocha wake George Lwandamina alibadili baadhi ya wachezaji kwenye kikosi kilichocheza na Simba.
Ruvu Shooting ambayo kwa matokeo haya inazidi kujipalia makaa kwani inabaki na pointi zake 28 katika nafasi ya 10, jana ilijitutumua kufanya mashambulizi ya hapa na pale hasa katika dakika ya 35 ambapo mchezaji mkongwe kwenye Ligi Kuu Shaaban Kisiga nusura aandike bao lakini shuti lake lilipanguliwa na kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’.
Katika dakika ya 75, Shaaban Msala aliikosesha tena Ruvu bao akiwa kwenye nafasi nzuri baada ya kuwalamba chenga mabeki wa Yanga lakini akapiga mpira nje.
Kikosi cha Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’, Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Vincent Bossou, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Justine Zulu/Juma Mahadhi dk78, Simon Msuva, Deus Kaseke/Emmanuel Martin dk78, Amisi Tambwe, Obrey Chirwa na Geoffrey Mwashiuya/Juma Said ‘Makapu’ dk63.
Ruvu Shooting: Bidii Hussein, Yussuf Nguya, Baraka Mtuwi, Damas Makwaiya, Said Madega, Kassim Dabi, Jabir Aziz, Shaaban Kisiga, Issa Kanduru/Fully Maganga dk46, Chande Magoja/Shaaban Msala dk49 na Abrahman Mussa.
Mwisho.