KAMATI ya nidhamu ya Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) imemfungia mechi 10 pamoja na faini ya Sh. 300,000 Kocha
wa timu ya Polisi Tabora kwa kosa la kumtukana mwamuzi wakati
wa mechi kati ya timu yake na Panone FC iliyochezwa mjini Moshi.
Maamuzi hayo yalitolewa jana baada ya kamati hiyo kukaa Februari 3, mwaka huu na kusikiliza mashauri 12 na kuyatolea hukumu huku mengine yakiendelea kusikilizwa.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF Boniface Wambura alisema Kocha huyo Eliakim Christopher amefungiwa kwa mujibu wa kanuni ya 39(2) ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baada ya kutiwa hatiani.
Mbali na adhabu ya kocha huyo, imewafungia
mechi tatu pamoja na faini ya Sh. 300,000 wachezaji wanne wa timu ya JKT Oljoro
kila mmoja.
Wachezaji hao Dihe Makonga, Swaleh Idd Hussein, Ramadhan
Mnyambegu na nahodha Shaibu Nayopa wamekutwa
na kosa la kuhusika na vurugu kwenye mechi dhidi ya Burkina Faso iliyochezwa
Morogoro pamoja na kumpiga mwamuzi katika moja ya mechi yao ya Ligi Daraja la
Kwanza.
Aidha, Mtunza
Vifaa wa JKT Oljoro FC, Eliud Mjarifu
amefungiwa miezi sita na kupigwa faini ya sh. 200,000 kwa kumpiga Kocha wa
Burkina Faso, CR Mwakambaya kwenye mechi kati ya timu hizo iliyofanyika Uwanja
wa Jamhuri mjini Morogoro.
Pia, Mjarifu amepewa
onyo kali na kutakiwa kutorudia tena kutenda kosa, kwani hata mwenendo wake
wakati wa shauri hilo ulionyesha utovu wa nidhamu mbele ya Kamati.
Wengine waliofungiwa mwaka mmoja ni viongozi wawili wa Chama cha Soka la Wanawake Tanzania (TWFA) Mkoa wa Mwanza kwa kuwashawishi wachezaji wa Mwanza Queens kugomea uamuzi halali.
Sophia Tigalyoma
(Mwenyekiti) na Katibu wake Hawa Bajanguo walitiwa hatiani kwa kuwashawishi
wachezaji kugomea uamuzi wa Kamati ya ya Soka la Wanawake (TFF) kutupa rufani
yao dhidi ya Kigoma.
Naye Mtunza
Vifaa wa Rhino Rangers FC, Albert Mbuji amefungiwa miezi sita na faini ya sh.
200,000 kwa kupatikana na hatia ya kuwatukana na kugomea uamuzi wa marefa
kwenye mechi dhidi ya Polisi Dodoma. Adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa
kanuni ya 40(2) ya FDL.
Wambura alisema
Kamati hiyo pia imeondoa malalamiko dhidi ya Ofisa Habari wa Ruvu Shooting,
Masau Bwire kwa vile refa Israel Mujuni Nkongo ambaye ni mlalamikaji hakufika
kwenye shauri hilo.
Nkongo alimlalamikia
Bwire akidai alitoa maneno yenye kuweza kuchochea chuki dhidi yake kwa waamuzi,
kwani kupitia redio 100.5 Times FM, Bwire alidai refa huyo ndiye aliyeshinikiza
kuondolewa kwa refa Mohamed Theofil kwenye ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).
Pia, Kamati hiyo
imemkuta bila hatia Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Singida (SIREFA), Gabriel Gunda
ambaye TFF ilimlalamikia kuwa akiwa Mtendaji Mkuu wa chama hicho alishindwa
kuhakikisha timu ya Singida inaingia uwanjani kucheza na Dodoma kwenye mechi ya
Kombe la Taifa kwa Wanawake.
Kamati ilikubaliana
na utetezi wa Gunda kuwa jukumu la timu hiyo lilikuwa mikononi mwa viongozi wa
TWFA Singida, na tayari SIREFA kupitia Kamati yake ya Nidhamu ilishatoa adhabu
kwa viongozi wa timu hiyo kutokana na kitendo hicho.
Nayo malalamiko ya
Polisi Tabora FC kutaka mechi yao dhidi ya Toto Africans FC irudiwe kwenye
uwanja huru kwa madai ya kuchezeshwa
zaidi ya muda unaotakiwa, na kutokuwepo ulinzi wa kutosha kwenye Uwanja wa CCM
Kirumba jijini Mwanza yamekataliwa.
Pia, Kamati ya
Nidhamu imeelekeza malalamiko ya timu za Mwadui FC na Polisi Mara FC dhidi ya
Toto Africans kwa kumchezesha mchezaji Ladislaus Mbogo bila kuonyesha leseni
yake yasikilizwe haraka na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kwa vile si ya
kinidhamu.
Kamati hiyo
iliendelea na kikao chake jana
kusikiliza malalamiko mengine ya kinidhamu yaliyofikishwa mbele yake.
No comments:
Post a Comment