Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Friday, November 25, 2016

LWANDAMINA AKUBALI BENCHI LA UFUNDI YANGA









KOCHA Mkuu mpya wa Yanga, George Lwandamina  amekanusha taarifa za kuleta wachezaji toka Zesco lakini pia amekiri wachezaji wa Tanzania ni legelege ukilinganisha na Zambia.
Lwandamina aliyasema hayo jana wakati akitambulishwa rasmi kwa wandishi wa habari pamoja na Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, Hans Pluigm.
Lwandamina alisema hana mpango wa kubadilisha chochote kwenye benchi la ufundi pamoja na wachezaji huku akikanusha kuwaleta nchini wachezaji Jesse Were na Misheck Chaila lakini akasema amekabidhiwa jukumu zito ila analichuliwa kama changamoto kuhakikisha Yanga inafanya vema.
 “Nitapambana kuhakikisha Yanga inafanya vizuri, najua ni changamoto mpya kwangu lakini nitafanya kila linalowezekana kuhakikisha tunafanya vizuri kuanzia kwenye ligi ya nyumbani hadi klabu Bingwa Afrika,” alisema Lwandamina
"Nasikia tetesi kuhusu wachezaji wapya kutoka Zesco kusajiliwa Yanga naomba ifahamike kuwa kama kocha mkuu sijui chochote labda mchakato hiyo inafanyika bila mimi kushirikishwa na kikosi kilichopo ndicho nitaendelea nacho" alisema Lwandamina.
Pia Lwandamina alisema hakuna wachezaji, aliowaleta japo amekiri wachezaji wa Tanzania hawako fiziki kama wa Zambia kwani alishawaona wakati wakicheza na Ruvu Shooting kwenye mechi ya mwisho ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara
Akimzungumzia mtangulizi wake Lwandamina amemsifu Pluijm kwa kusema amefanya kazi nzuri na kuahidi kufuata nyayo zake kwa kushirikiana naye bega kwa bega kuhakikisha Yanga inapata mafanikio zaidi.
Nae Mkurugenzi mpya wa ufundi Pluigm alisema yeye hana shida na kubadilishiwa majukumu kikubwa ataendelea kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba wake.
Pluigm alianza kuifundisha Yanga 2014 na ameiongoza katika mechi 128 kwenye awamu mbili, akishinda 80, sare 25 na kufungwa 23.
Katika mechi 19 za nusu msimu mwaka 2014, alishinda 11, sare sita na kufungwa mbili, wakati katika mechi 110 za tangu mwaka jana, alishinda 69, sare 19 na kufungwa 21.
Na anahama nafasi akiwa akibeba mataji yote matatu msimu uliopita, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
Pluijm pia aliiwezesha Yanga kufika hatua ya makundi ya michuano ya Afrika (Kombe la Shirikisho) kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998 na mara ya pili kihistoria.
Yanga ilifika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka huu baada ya mwaka 1998 kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
Na kwa mafanikio hayo, Pluijm alishinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita. 

No comments:

Post a Comment