Limekuwa jambo la kawaida kuwasikia watani wa jadi Simba na Yanga kufanya mambo ambayo mpinzani mmoja anakuwa anafanya na sasa linalosubiriwa kwa hamu ni kuona kama Yanga watawaiga Simba baada ya wao kukubaliana kufanya mabadiliko ya mfumo ambao wanautumia sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mkutano wa Yanga ambao umeitishwa kwa dharula na mwenyekiti wa timu, Mratibu wa matawi ya Yanga na Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Yanga, Omary Kaaya alisema jambo hilo linauwezekano wa kujadiliwa katika mkutano wa kesho ila tu endapo mwenyekiti atataka kulizungumzia.
“Kama tumevyosikia majirani nzetu kuna wenzetu kuna mtu anataka kuwekeza ili kuona kama wanaweza kupata mafanikio baada ya kuona sisi tunakuwa na mafanikio na kweli hilo ni jambo ambalo linahitaji kufanyiwa mabadiliko ya kimfumo,
“Kama kutakuwa na maoni ya wanachama ambao wanataka na sisi kuwepo na mtu ambaye anataka kufanya kama MO anavyotaka kufanya kwa Simba basi mwenyekiti atalizungumzia hilo maana imeshakuwa kawaida jirani akifanya jambo mwingine na yeye analifanya,” alisema Kaaya.
Aidha Kaaya alizitaja ajenda za mkutano wa kesho kuwa ni 1.Mwenendo wa Timu, 2.Mahusiano kati ya Yanga na TFF, 3.Katiba ya Yanga, 4.Mapato na Matumizi ya Klabu, 5.Shukrani kwa Wajumbe waliomaliza muda wao, 6.Kuishukuru Serikali kwa ushirikiano wanaonyesha kwenye mashindano tunayoshiriki, 7.Maendeleo ya klabu na 8.Mengineyo.
Pia katika hatua nyingine Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Habari wa Yanga, Jerry Muro amesema kuwa amerejea kazini kuendelea na kazi baada ya kumaliza likizo yake na kutuma ujumbe kwa TFF kuwa amepata barua yao lakini bado anahitaji barua ya hukumu.
“Niombe kupta nakala ya hukumu tuisome na tujue wametumia sheria gani na kanuni gani ambazo wametumia kunihukumu na baada ya hapo tutaangalia kama tunakata rufaa au tunaacha kwahiyo niwatumie taarifa ndugu zangu wa TFF kuwa wajue nimerudi,” alisema Muro.