Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, August 24, 2016

NGAWINA NA SALVATORI WAANZISHA KLINIKI

KIUNGO wa zamani wa timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ngawina Ngawina, pamoja na kiungo wa zamani wa Yanga, Salvatory Edward wameanzisha kituo cha kuibua vipaji vya wanasoka chipukizi chini ya umri wa miaka 17 na kuviendeleza.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ngawina alisema kituo chao kinaitwa Kambiasso Sports na kwamba kwa kuanzia Jumamosi wiki hii watafanya kliniki maalum ya kusaka vipaji hivyo kwenye Uwanja wa Tandika Mabatini, Dar es Salaam, dhamira yao kubwa ikiwa ni kuhakikisha wachezaji wenye vipaji wanaendelezwa na kutafutiwa timu.
“Kila mzazi mwenye mtoto ambaye anaamini ana kipaji cha soka na anahitaji aendelezwe, amlete mwanae Tandika Mabatini Jumamosi Agosti 27,  ajitahidi saa mbili asubuhi awe ameshafika, kwani ndiyo muda tutakaoanza.
“Kliniki yetu itaendeshwa na makocha mahiri, ambao wana leseni za ukocha kutoka CAF (Shirikisho la Soka Afrika), ili kufanya hili jambo kiuweledi zaidi na kupata vijana wenye sifa,” alisema Ngawina.
Alisema dhamira yao ni kupata vijana wengi wenye vipaji kadri iwezekanavyo na kwamba suala la idadi itategemea na watakavyoona siku hiyo, lakini dhamira yao ni kuwa na vijana wasiopungua 30, lakini si lazima wote wapatikane Dar es Salaam, wataenda hadi mikoani.
Aliwataja watakaoendesha mshujo huo licha ya yeye na Salvatory, pia atakuwepo kocha Kennedy Mwaisabula, ambaye amepata kufundisha timu mbalimbali nchini ikiwemo Yanga.
Mwingine ni kipa wa zamani wa timu mbalimbali ikiwemo Simba ya Dar es Salaam na Ferroviario De Maputo ya Msumbiji, Muharami Mohammed ‘Shilton’, ambaye kwa sasa ni kocha wa makipa wa timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ . Pia atakuwepo kocha mwingine wa makipa Terry Muhorel.
“Soka si kama paa la nyumba kwamba siku zote linakuwa juu tu. Soka inaanzia chini na ndiko tunakotaka twende,” alisema Ngawina.
Kwa upande wake Salvatory alisema dhamira yao ni kuwa na kituo ambacho kitakuwa hazina ya nchi kwa wachezaji wa siku za usoni, lakini pia kiwe kitovu cha timu mbalimbali kuchukua wachezaji.
“Tunaamini vijana wetu wakishaiva tutawauza timu mbalimbali za ndani ya Tanzania na nje, kwani kituo kina uhusiano mzuri na watu mbalimbali waliopo hapa nchini na hata nje ya nchi,” alisema Salvatory.
 “Tunaosimamia jambo hili tumecheza mpira kwa kiasi cha kutosha, tumesomea ukocha, tunajua nini cha kufanya kuendeleza vijana wetu,” alisema.

Aliwaomba wachezaji chipukizi wa umri huo wanaoamini wana uwezo wajitokeze siku hiyo ili kuwania nafasi ya kuwepo katika kituo hicho ambacho kitakuwa Temeke, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment