TIMU
ya soka ya Taifa, Taifa Stars leo imewatoa mashabiki wa soka vichwa chini
baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya miamba ya Afrika, Algeria katika
mechi ya kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2018, kwenye Uwanja wa Taifa
Dar es Salaam.
Matokeo
hayo sasa yanaifanya Stars ipigane kufa kupona mjini Algiers katika mechi ya
marudiano Jumatano ijayo.
Stars
ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 mpaka dakika ya 70, lakini ikaruhusu Algeria
kusawazisha mabao hayo ndani ya dakika nne.
Ikicheza
mbele ya umati uliokusanyika kwenye uwanja huo wa Taifa, Stars ilitandaza soka
safi katika kipindi chote cha kwanza huku wachezaji wake wakikosa mabao kadhaa.
Mabao
ya Stars yalifungwa katika kila kipindi kupitia kwa Elias Maguli katika dakika
ya 43 na Mbwana Samatta katika dakika ya 54.
Maguli
alifunga bao la kuongoza baada ya kuunganisha mpira wa kurusha wa Haji Mwinyi
kabla ya kuichambua ngome ya Algeria na kuujaza mpira wavuni.
Samatta,
ambaye ni mfungaji bora Afrika kwa sasa, alifunga bao lake kwa shuti.
Dakika
ya 65 benchi la ufundi la Stars lilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Mudathir Yahya
na Maguli na nafasi zao kuchukuliwa na Said Ndemla na Mrisho Ngassa.
Mabadiliko
hayo ndiyo yaliyoigharimu timu, kwani sasa ilionekana kupwaya zaidi na Slimani Islam wa Algeria alitumia nafasi hiyo
kusawazisha mabao yote mawili katika dakika ya 71 na 75 baada ya kuwazidi
maarifa mabeki wa Stars.
Mbali
na kasoro hizo, Stars ilianza mchezo huo kwa kasi ya kushambuliana katika
dakika ya pili tu ya mchezo Farid Musa alipata nafasi nzuri ya kufunga
akapaisha.
Nafasi
nzuri za kufunga kama hizo pia zilipatikana kwa Samatta na Thomas Ulimwengu kwa
nyakati tofauti, lakini ama walikuwa wakipaisha au mipira ilidakwa na kipa wa
Algeria M’bolhi Rais.
Stars
inatarajiwa kuondoka nchini kesho kuelekea Algiers kwa ajili ya mechi ya
marudiano itakayochezwa Jumatano ambapo timu itakayoshinda itaingia kwenye
makundi katika kinyang’anyiro hicho cha kuwania kwenda Urusi.
Stars:
Ally Mustapha, Shomari Kapombe, Haji Mwinyi, Nadir Haroub, Kelvin Yondani,
Himid Mao, Thomas Ulimwengu, Mudathir Yahya/Said Ndemla, Mbwana Samatta, Elius
Maguli/Mrisho Ngassa, Farid Musa.
Algeria:
M’bolhi Rais, Mandi Issa, Ghoulam Faouzi, Mesloub Wald, Medjani Carl, Zeffane
Mehdi, Guediora Aldane, Taider Saphir/Belkarou Hichem, Belfodil Isha/Bentaleb
Nabil, Slimani Islam, Mahrez Ryad.
No comments:
Post a Comment