KAMPUNI ya Azam Media
imezindua chaneli mpya ya ‘Azam Sports HD’ itakayojihusisha na matangazo ya
michezo.
Kuzinduliwa kwa
chaneli hiyo ni moja ya mpango wa kampuni ya Azam media kujikita katika utoaji
wa burudani kwa wapenzi wa michezo mbalimbali na wateja wa kampuni hiyo.
Akizungumza katika
hafla ya uzinduzi wa chaneli hiyo, Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Rhys Torrington
alisema kuwa wateja wote wanaotumia huduma za tetelevisheni ya Azam na
waliolipia moja ya vifurushi vya dikoda yao watapata huduma hiyo kwa kuongeza
malipo ya Sh. 15,000.
“Uzinduzi wa huduma
yetu mpya ya chaneli ya Azam Sports HD ni hatua mojawapo ya mikakati yetu ya
kuwapatia wateja wetu burudani ya michezo. Kila mtu anayetumia huduma zetu
atapata fursa ya kuangalia michezo yote inayofanyika duniani,” alisema
Torrington.
Alisema huduma hii ni
ya wateja wote wanaopatikana Tanzania na kwa watumiaji wengine waliopo nje ya
Tanzania hawataweza kuipata hadi hapo baadae.
Torrington alisema chaneli
hii kwa kuanza itaonesha moja kwa moja mashindano ya mpira wa miguu wa kombe la
La Liga na VPL ambapo inatarajiwa kuanza Agosti 21 mwaka huu kwa kuonesha
pambano la mpira wa miguu katika ya timu ya Malaga na Seville.
Kwa upande wake Naibu
Mtendaji wa kampuni hiyo, Tido Mhando alisema kuwa pamoja na kuonesha mapambano
mbalimbali ya mpira wa miguu, chaneli hiyo pia itaonesha aina zingine za
michezo kama vile mpira wa kikapu, mashindano ya magari na kuogelea.
“Tumeazimia kuwa watoa
burudani wa uhakika kwa wateja wetu kwa kuwaletea karibu michezo yote
waipendayo kupitia chaneli yetu hii mpya tuliyoizindua leo. Tutaanzia
hapa nyumbani kwa kuonesha mapambano mbalimbali hadi ulaya na mabara mengine,”
alisema Mhando.
Mhando alisema kuwa chaneli
hiyo itaongozwa na watangazaji mahiri na wenye uzoefu wa kutosha katika fani ya
utangazaji wa michezo na hivyo wananchi watarajie kupata burudani isiyo na
kifani.
Aidha Mhando alisema chaneli
hiyo itakuwa na vipindi vya uchambuzi wa kina wa michezo utakaoongozwa na
wachambuzi waliobobea katika kazi hiyo ikiwemo Ally Mayay, Hussein Sappy,
pamoja na Edo Kumwembe
No comments:
Post a Comment