Brendan Rogers atoa sababu za kufungwa na United katika International Champions Cup. |
Meneja wa klabu ya Liverpool Brendan Rodgers, ameelezea hisia zake baada ya kupoteza mchezo wa hatua ya fainali ya michuano ya International Champions Cup dhidi ya Man Utd uliochezwa usiku wa kuamkia hii leo mjini Miami nchini Marekani.
Rodgers, amesema matokeo ya mchezo huo hayajamvunja moyo wa kuendelea kukiamini kikosi chake ambacho August 16 kitaanza mshike mshike wa kusaka ubingwa wa nchini Uingereza, baada ya kukosa nafasi ya kutawazwa kuwa mabingwa msimu uliopita.
Amesema kikosi chake hakikucheza vibaya katika mchezo huo ambao ulihudhuriwa na mashabiki wengi, lakini makosa madogo madogo yaliwafanya wachezaji wake kujikuta wakiadhibiwa na Man Utd kwa kufungwa mabao matatu kwa moja.
Katika mchezo huo Liverpool walikuwa wa kwanza kupata bao kwa njia ya mkwaju wa penati uliopigwa na kiungo na nahodha Steven Gerrard lakini Man Utd waligeuka na kupata mabao matatu yaliyopachikwa wavuni na Wayne Rooney, Juan Mata pamoja na Jesse Lingard.
Katika hatua nyingine meneja huyo kutoka Ireland ya Kaskazini ameahidi kufanya usajili wa mchezaji mmoja ama wawili katika kipindi hiki cha kuelekea mwanzoni mwa msimu wa ligi.
Wachezaji ambao wanadhaniwa huenda wakawa njiani kujiunga na klabu hiyo ya Anfield ni beki wa kuliwa kutoka nchini Hispania na klabu ya Atletico Madrid Javier Manquillo pamoja na Alberto Moreno Pérez anaecheza nafasi ya beki wa kushito kwenye klabu ya Sevilla.
Wakati huo huo, Rodgers amethibitisha kiungo mshambuliaji kutoka nchini Brazil Philippe Coutinho, anakaribia kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu ya Liverpool baada ya kuonyesha kiwango kizuri tangu aliposajiliwa akitokea Inter Milan.
No comments:
Post a Comment