Baada ya kujaribu bila mafanikio kulitwa kombe la kandanda la dunia
tangu walipofanya hivyo mara ya mwisho mwaka 1990, hatimaye ndoto ya
vijana wa Jogi (timu ya taifa ya Ujerumani) ilitimia usiku wa Jumapili.
Mchezaji kiungo Mario Goetze --Super Mario-- alijiandika kwenye vitabu
vya historia pale alipopachika goli la ushindi katika fainali za kombe
la dunia, lililoipatia Ujerumani ubingwa wa dunia. Nyota huyo wa klabu
ya Bayern Munich alitegua kitendawili cha ubingwa katika dakika ya 113
na kuinyamanzisha Argentina, huku ndoto ya Lionel Messi ya kufuata nyayo
za nguli Diego Maradona ikiishia kwa kushindwa.
Ushindi mtamu
Ujerumani sasa imeshinda kombe la dunia mara nne, na kulifanya taifa
hilo kubwa duniani kuwa nyuma tu ya Brazil yenye rekodi ya ushindi mara
tano. Muda wa maamuzi wa fainali hiyo iliyojawa na msisimko na magoli
yaliyofungwa kwa ustadi mkubwa ulikuja wakati timu hizo zikinyemelewa na
mikwaju ya penati mbele ya watazamaji 74,738 katika uwanja maarufu wa
Maracana mjini Rio de Janeiro.
Mchezaji bora wa mechi hiyo ya fainali Goetze aliituliza kifuani krosi
ya Andre Schuerrle na bila kufanya ajizi akasukuma mkwaju uliyomduwaza
mlinda mlango wa Argentina Sergio Romero, kwa goli la ushindi
lililomfanya nahodha Philip Lahm kubeba kombe la dunia.
"Siamini kama sisi ndiyo mabingwa wa dunia. Suala la iwapo tuna mchezaji
bora mmoja mmoja halijalishi hata kidogo, kilichomuhimu ni kuwa na timu
bora. Tumekuja tukiboresha mchezo wetu wakati wote wa mashindano, na
hatukukata tamaa pale mambo yalipotuendea vibaya, tuliendelea kushika
njia yetu, na mwishowe tumesimama hapa kama mabingwa wa dunia. Ni hisia
isiyoelezeka," alisema nahodha wa timu hiyo Philip Lahm
Baada ya kosa kosa za miaka mingi
Ujerumani ambayo iliinyeshea Brazil mvua ya magoli 7 -1 katika mchezo wa
nusu fainali, imekuwa timu ya kwanza ya Ulaya kubeba kombe la dunia
katika Amerika ya Kusini. Walianza kushinda taji hilo mwaka 1954, na
kulirudia mwaka 1974 na 1990. Wamekuwa wakilikosakosa ama kwa kutolewa
kwenye hatua ya nusu fainali au fainali katika miaka ya hivi karibuni.
Taji hilo ni matokeo ya mbadiliko katika mfumo mzima wa soka ya
Ujerumani mwanzoni mwa karne hii, na kutawazwa kwa kizazi cha dhahabu
kikiongozwa na Lahm na Bastian Schweinsteiger, kama alivyosema kocha wa
Ujerumani Joachim Loew.
"Ninaamini kazi hii ilianza tangu miaka 10 iliyopita na Juergen Klinsman
na sisi tulifanya kuendeleza kile alichokianzisha. Tumefanya kila kitu
kuhakisha tunafika siku hii. Timu yetu imefanya kazi kubwa sana, imekuwa
na hamasa kubwa na hasa katika wiki hii ya mwisho, kila mchezaji
amejituma na ndiyo maana tumeweza kushinda fainali hii hapa."
Kina Messi wajilaumu wenyewe
Argentina ambao walishinda taji hilo mwaka 1978 na 1986 kwa kuifunga
Ujerumani, wamemaliza wakiwa washindi wa pili kama ilivyokuwa mwaka 1930
na 1990, na nyopta wao Lionel Messi hakucheza kama alivyotarajiwa.
Kiungo wa kati Javier Mascherano alisema ni vigumu kueleza, kwani
walifanya kila kitu kushinda na walikuwa na nafasi nzuri zaidi.
Messi, Gonzalo Higuain na Rodrigo Palacio walikosa nafasi nzuri cha juu
wakati kichwa cha Benedikt Hoewedes kiligonga mwamba kwa upande wa
Ujerumani mbele ya maefu ya mashabiki wakiwemo rais wa Ujerumani Joachim
Gauck, Kansela Angela Merkel, rais wa Urusi Vladmir Putin na mwenyeji
wao rais wa Brazil Dilma Roussef.
Upinzani usiotarajiwa
Ujerumani ilimiliki mpira kwa sehemu kubwa kama ilivyotarajiwa huku
mashabiki wake wakiipa morali ya nyimbo za "ole", lakini Argentina
ilionyesha upinzani mkali tofauti na ilivyokuwa katika mchezoi wa nusu
fainali na Uholanzi. Tofauti na robo fainali dhidi ya Ufaransa, na nusu
fainali dhidi ya Brazil, Ujerumani ilishindwa kupata goli la mapema
dhidi ya safu imara ya ulinzi ya Argentina, ambayo ilikuwa haijafungwa
katika michezo mitatu ya mwisho ya mtoano, na ilikuwa na haiba tofauti
na Brazil.
Wakiwa wamebeba kombe mikononi mwao, wachezaji wa Ujerumani waliimba
pamoja na mashabiki wao, wimbo maarufu wa Am Tag Wie Diesen (Katika siku
kama hii) uliyopigwa na bendi ya Ujerumani ya Die Toten Hosen na
kuchezwa uwanjani. Ilikuwa ndoto iliyotimia baada ya subira ya miaka
mingi.
No comments:
Post a Comment