Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, August 27, 2023

TAMASHA LA KITAIFA LA UTAMADUNI, NYENZO MUHIMU YA UZALENDO


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Fatuma Mtanda (wa pili kushoto) alipotembelea banda la Mkoa wa Mtwara baada ya kufungua Tamasha la Kwanza la Kitaifa la Utamaduni kwenye Uwanja wa Uhuru, Temeke Mkoani Dar es Salaam, 2022.


   

Wasanii kutoka Mkoa wa Mwanza wakicheza ngoma ya nyoka katika Tamasha la Kwanza la Kitaifa la Utamaduni lililofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, 2022.

Na Rahel Pallangyo 

SAFARI kubwa ya mageuzi ya kuimarisha utamaduni wa Mtanzania imepamba moto kwa kuwepo kwa tamasha kubwa la Kitaifa la Utamaduni. Tamasha hili lilioanza mwaka jana na mwaka huu kuingia mwaka wake wa pili ni utekelezaji wa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha jamii inajifunza na kurithishwa tamaduni kwa kizazi kijacho. 

Tamasha hili ambalo mwaka jana lilifunguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam linaleta mwamko mpya wa kiutamaduni ambao unajenga umoja kwa kuwaleta Watanzania pamoja kwa wakati mmoja. Uwepo wa pamoja unawezesha hata wale wasiojua utamaduni wao kupata fursa ya kujifunza, ikiwa ni ukurasa mpya kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. Tamasha la kwanza la kitaifa lilifanyika Dar es Salaam kuanzia Julai 1-7, 2022 na mwaka huu linafanyika Njombe kuanzia  Agosti 25-27 katika viwanja vya Sabasaba likibeba kaulimbiu isemayo ‘Utamaduni ni msingi wa maadili, tuulinde na kuuendeleza’. 

Wakati akisimikwa kuwa Mkuu wa Machifu Tanzania mkoani Mwanza, Septemba 8, 2021 na kufunga Tamasha la Utamaduni lililoandaliwa na Umoja wa Machifu Tanzania na kuitwa Chifu Hangaya likiwa na maana ya nyota ya asubuhi inayong’aa, Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza kuendelezwa kwa utamaduni kwa manufaa ya taifa hili na kulipeleka kwenye nidhamu na woga unaotakiwa katika maisha. Msisitizo wake wa kuwa na matamasha ya kitamaduni ulirejewa Januari 2022 wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye tamasha la kihistoria la Utamaduni la Mkoa wa Kilimanjaro lililofanyika katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi. 

Kuwapo kwa maono ya Rais Samia katika hili ni kutekeleza pia maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye alisema taifa lisilo na utamaduni wake ni Taifa mfu. Kwa kuwa utamaduni ni dhana pana kwani ni uhai na kielelezo cha kabila au nchi yoyote duniani, kwani utamaduni ni mfumo wa maisha ya watu jinsi wanavyoishi na maendeleo yao kijamii, kiuchumi, kisiasa kuhimizwa kuwa na matamasha ni sehemu mojawapo ya maana katika kufungamanisha taifa. 

Pamoja na Tanzania kuwa na zaidi ya makabila 120 yenye mila na desturi zao tofauti katika misingi ya maadili na uwajibikaji na hapa ndipo unapoona umuhimu wa kurithisha vizazi vipengele muhimu vya utamaduni ambavyo vitawafanya kujitambua na kuthamini uwapo wao na kuona namna ya kuviendeleza wao na vizazi vyao.

 Katika mazingira ya usasa zaidi huku masimulizi mengi yakitoweka, uwapo wa matamasha unasaidia kutunza utamaduni wa taifa hili ikiwamo heshima iliyopo miongoni mwa jamii, utunzaji wa watoto, wazee, vijana na walemavu pia ni mavazi ya heshima ambayo kila mtu anapaswa kuvaa yasiyovunja maadili ya taifa. Tunaweza kujikumbusha kwamba mwaka 1964 wakati Chama cha TANU kikisherehekea miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, Rais wake Mwalimu Julius Nyerere alitoa hotuba iliyokuwa na ujumbe mahususi kwa watoto wa Tanzania kuhusiana na suala la utamaduni na vipengele vyake. 

Mwalimu Nyerere anasema: “...watoto wote wanaosoma shuleni na wale wasiokuwa na bahati hiyo, yawapasa kujifunza kazi za asili za wazee wetu. Mjifunze kwa wazee wenu na babu zenu hadithi, mashairi na historia ya watu wetu maana mambo mengi hayakuandikwa vitabuni na kama hamkuyajua basi yatasahaulika.” Aliongeza: “Hadithi hizi ni sehemu ya urithi wetu, ni lazima mzijue na kuwafundisha wengine pia wazijue zisisahaulike kizazi hata kizazi.”

Kwa kuwa mengi yaliyokuwa yakitolewa na wazee kwa njia ya masimulizi hayakuwa yakiandikwa, njia kubwa na rahisi ya kuyarithisha ilikuwa ni kwa mapokeo kwa wakati huo yaani kurithishwa kutokana na masimulizi ya wazee. Mwalimu Nyerere aliwasisitiza watoto kupata urithi huo kutoka kwa wazee wao maono yake yamekuja kuungwa mkono na Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan baada ya kuvaa viatu vyake na kuanzisha Tamasha la kitaifa la utamaduni ambayo hufanyika kila mwaka. Tanzania ina matamasha mengi pamoja na ya kikabila pia yapo matamasha ya muziki, filamu na matamasha ya utamaduni ikiwamo vyakula na mila.

 Matamasha haya yote ni utekelezaji wa Sera ya Utamaduni ambayo imetoa mwelekeo wa maendeleo ya utamaduni kwa kuainisha jinsi shughuli za utamaduni zitakavyoendeshwa na kusimamiwa pamoja na kuweka wazi majukumu ya serikali, wananchi kwa makundi au mmoja mmoja na sekta binafsi ili kufanikisha lengo la kuhifadhi na kuuenzi utamaduni. 

Tamasha la kitaifa lenye mwaka wa pili sasa ni mwendelezo wa nia thabiti ya viongozi wa taifa hili la kuwa na maendeleo yanayozingatia mila, desturi na kuheshimu maadili na uwajibikaji. Safari ya mageuzi ya kuimarisha utamaduni na kuwa darasa kwa vijana wanaokua, kwani tamasha liliwezesha wananchi kukutana nchi nzima na kuwa wamoja, wasiojua utamaduni wao watapata fursa ya kujifunza, ikiwa ni ukurasa mpya kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. 

Tamasha ni mwanzo mzuri wa safari ya kuimarisha utamaduni kwa kuwa yatainua na kuibua hazina kubwa ya kiutamaduni miongoni mwa jamii nchi nzima na yana tija kwa kuleta taifa pamoja hasa kizazi cha sasa kujua chimbuko lao na vyakula vya makabila na mila na desturi zao. Tamasha linajumuisha shughuli za utamaduni ambazo ni maonesho ya ngoma na vyakula vya asili na matembezi ya kiutamaduni na mavazi ya utamaduni ambavyo hufanya wananchi kufurahia kuona tamaduni zao kwa wakati mmoja katika matukio ya kijamii.

 Akizungumzia tamasha hilo la kitaifa, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Yusuf Yakubu alisema matukio haya yamefungua historia mpya ya nchi na kuyatumia ili kutangaza nchi. “Huu ni mwanzo mzuri wa kutumia utamaduni katika kuitangaza nchi yetu. Serikali inaendelea kushirikiana na kufanya kazi na makabila yote nchini ili kuendeleza mila njema kwa vizazi vijavyo. 

 Utamaduni ni hazina ambayo kila kabila na taifa wanapaswa kuulinda na kuendeleza kwa kizazi hadi vizazi vijavyo,” alisema. Yakubu anasema kuna shughuli mbalimbali za utamaduni hufanyika ikiwemo ngoma na maonesho ya vyakula na historia mbalimbali za makabila ya Tanzania katika tamasha hilo la kitaifa. “Kimsingi tamasha hili limejumuisha vitu vikubwa vitatu, shughuli za utamaduni ambazo ni maonesho ya ngoma na vyakula vya asili, matembezi ya kiutamaduni, usiku wa taarabu na maadhimisho ya siku ya Kiswahili.”

 Kwa kuwa utamaduni ni hazina ya nchi serikali kwa kuendelea kushirikiana na kufanya kazi na makabila yote nchini ili kuendeleza mila njema kwa vizazi vijavyo itakuwa inahifadhi tunu hii muhimu kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. 

Katika mahojiano Yakubu anasema katika hili viongozi wa kimila na machifu hawana budi kusimamia mila na desturi njema kwa watoto na kuongeza serikali inathamini utamaduni wa taifa kwa kuzingatia kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema: “Utamaduni ni kiini ama roho ya taifa lolote, taifa lisilo na utamaduni ni sawa na mkusanyiko wa watu usio na roho.” “Kila mmoja wetu anawajibu wa kulinda utamaduni, kuendeleza na kuuhifadhi ndiyo maana tunasema ‘Utamaduni wetu; Fahari yetu’,” aliongeza.

No comments:

Post a Comment