Tuesday, February 25, 2014
CHOLO:HAKUNA MGOMO SIMBA BALI NI MATOKEO YA MECHI
NAHODHA wa Simba Nassoro Cholo amesema kufanya kwao vibaya kwenye mechi mbalimbali za Ligi Kuu hakumaanishi kuwa wachezaji hawajitumi bali Ligi imekuwa ngumu kwa vile kila timu imejiandaa kufanya vizuri.
Kauli hiyo imekuja baada ya Simba kufanya vibaya kwenye mechi yao dhidi ya Ruvu JKT baada ya kutandikwa mabao 3-2 kwenye mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Chollo alisema ni muhimu wanachama wa Simba wakashikamana na kuwaunga mkono kipindi hiki kigumu kwao, ili kufanya vizuri katika michezo inayokuja.
Alisema ni haki ya wanachama kulalamika kwamba timu haifanyi vizuri kwasababu wana uchungu nao, lakini akawakumbusha kuwa sio kwamba wanapenda kufanya vibaya hata wao pia wanaumia isipokuwa matokeo siku zote hubadilika.
“Ni haki ya wanachama kuwalaumu wachezaji, viongozi lakini twende mbele na kufikiria kuwa katika mchezo siku zote usitegee kushinda, kuna kufungwa na kutoka sare pia, ndivyo ulivyo, tuko katika wakati mgumu,”alisema.
Cholo alihimiza wachezaji wanzake kujitambua katika kipindi hiki kigumu kwa kujitahidi kufanya vizuri katika mechi zijazo ili kubaki katika nafasi nzuri.
Kuhusu kutokuelewana kati yao na Kocha wao Zdravko Logarusic alisema anavyofundisha kwa mtu ambaye umelelewa katika utamaduni tofauti anapozungumza jambo wakati mwingine unaweza kuchukulia kama tusi lakini kumbe ndivyo Kocha alivyozoea.
Mchezaji huyo hakucheza katika mzunguko wa pili kutukana na kusumbuliwa na majeruhi ya mguu wa kushoto lakini kwa sasa amebainisha kuwa yuko fiti, hivyo inategemea katika mazoezi yake kama atachaguliwa kwenye kikosi kijacho kitakachoikabili Ruvu Shooting.
Naye Katibu Mkuu wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema kikosi hicho kinaendelea na mazoezi ili kuanzia mechi inayokuja dhidi ya Ruvu Shooting iweze kufanya vizuri na kuhakikisha wanabaki katika kiwango kizuri.
Wakati huo huo, Kamwaga aliwahimiza wanachama wa Simba kujitokeza Jumamosi asubuhi kwenye Ofisi hizo Makao Makuu, wakiwa na Jemba, Shona na vifaa vingine kwa ajili ya kwenda kutengeneza uwanja wao ulioko Bunju.
Alisema baada ya wanachama kutengeneza watapeleka greda kuuweka sawa na ndani ya siku 100 watakuwa wamemaliza kuweka nyasi bandia ili kuwawezesha wachezaji kuanza kuutumia kwa mazoezi mbalimbali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment