LONDON, England
KILA msimu wa Ligi Kuu England unadaiwa kuwa na mambo mengi ya kushangaza na ambayo hayakutarajiwa.
Mambo hayo yanatajwa kuwa miongoni mwa vitu vinavyoifanya ligi hiyo kuwa na msisimko wa aina yake.
Ukiangalia katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni ukianza na msimu wa 2008/2009, ilishuhudiwa timu iliyokuwa imesheheni vijana chipukizi, Hull City ikiungana na vigogo kileleni mwa ligi hiyo ikiwa ni baada ya kucheza mechi tisa, licha ya baadaye kujikuta ikining’inia kwenye mstari wa kushuka daraja.
Kama ilivyo kwa timu hiyo, pia msimu uliopita ilishuhudiwa West Brom nayo ikiwania nafasi ya kucheza michuano ya klabu Bingwa Ulaya baada ya kucheza mechi 19.
Hali hii pia inaonekana kutokuwa tofauti na msimu huu ambao kwa sasa inaonekana timu ya Liverpool inaonekana inaweza kuleta ushindani kwenye mbio za kuwania ubingwa wa ligi baada ya kushinda mechi tatu mfululizo za kwanza.
Mbali na timu hiyo, pia timu ya Crystal Palace, ambayo inawekwa kwenye kundi la kushuka daraja, nayo inaonekana huenda ikawa tishio tofauti na inavyoandikwa magazetini.
Msimu huu pia inatarajiwa vilevile baadhi ya wachezaji huenda wakaonesha viwango vyao na kuwa nyota katika timu zao kama ilivyokuwa msimu uliopita ambapo ilishuhudiwa wachezaji kama Michael Carrick, ambaye alikuwa akiachwa nyuma kwenye orodha ya wachezaji akitakata na kuwa miongoni mwa wachezaji waliotikisa kwenye ulimwengu wa soka.
Lakini hata hivyo wakati nyota huyo aking’ara, wapo wachezaji ambao walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri, lakini matokeo yake wakajikuta wakimaliza msimu huo vibaya.
Ifuatayo ni orodha ya wachezaji watano ambao msimu uliopita ulikuwa ni wa majanga kwao, lakini kwa sasa tangu ligi hiyo ianze kutimua vumbi wanaonekana huenda msimu huu wakazinduka na kufanya vizuri.
1.
Javi Garcia | Manchester City
Msimu uliopita Manchester
City iliingia kwenye upinzani mkubwa na mahasimu wao, Manchester United na
Arsenal katika mbio za kumwania Garcia kutoka
timu ya Benfica, zikiwa ni dakika
za mwisho kabla dirisha la usajili
halijafungwa.Kwa kufanikisha usajili huo wa pauni milioni 16, ilionekana kuwa ushindi mkubwa kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Roberto Mancini na huku Manchester City ikionekana kuimarisha zaidi kikosi chake kwa ajili ya kutetea ubingwa wake.
Hata hivyo mchezaji huyo alijikuta akiingia kwenye lawama kubwa baada ya kushindwa kuhimiri mikikimikiki ya Ligi Kuu.
Katika msimu wake wa kwanza ilishuhudiwa, Garcia akianza kikosi cha kwanza kwenye mechi 17 na huku ikishuhudiwa timu yake ikishindwa kutetea ubingwa wake.
Nyota huyo huku akiwa anafahamu ni nembo ya Mancini kwenye kikosi cha Etihad, lakini ukweli ni kwamba hakuna mchezaji ambaye huwa ni mbaya mara zote na mchezaji kama huyo ambaye alikuwa ametakataka akiwa na timu ya Benfica kwa misimu miwili haikutarajiwa kama angeshindwa kuhimili maisha ya Ligi Kuu ya England.
Hata hivyo inaelezwa kuwa katika msimu huu Mashabiki wa Man City wanatarajia kushuhudia pauni milioni 16 walizowekeza kwa mchezaji huyo zikizaa matunda.
2. Gylfi Sigurdsson |
Tottenham
Gylfi Sigurdsson alikuwa sehemu ya wachezaji nyota wa timu ya Swansea City ambao walitikisa kwenye michauno hiyo ya Ligi Kuu ya England katika msimu wa 2011//12.
Hadi mwishoni mwa msimu huo Swansea ilikuwa na pointi 47 ambazo ziliifanya imalize ligi ikiwa kwenye nafasi ya 11.Sigurdsson, ambaye alikuwa sehemu muhimu kwenye kikosi hicho, alikuwa akiichezea timu hiyo kwa mkopo wa muda mrefu akitokea klabu ya nchini Ujerumani, Hoffenheim.
Uwezo wake unadaiwa ndiyo uliomshawishi Kocha Brendan Rodgers kuanza harakati za kumsaka ili aweze kukipiga Liverpool, ingawa ilizidiwa maarifa na Tottenham ambayo ilifanikiwa kunasa saini ya raia huyo wa Iceland kwa pauni milioni 8.
Hata hivyo, baada ya kutua kwenye timu hiyo, Sigurdsson alijikuta akishindwa kufurukuta mbele ya Clint Dempsey na Moussa Dembele, baada ya msimu uliopita kuchezeshwa mechi 12 za kikosi cha kwanza cha Spurs.
Katika kikosi hicho, wakati Dempsey alipokuwa akicheza, Dembele alikuwa msaidizi wake na hali huenda ikawa mbaya zaidi kwa Sigurdsson baada ya kusajiliwa mchezaji mpya Roberto Soldado.
Inaelezwa kuwa hata hivyo endapo atapewa namba nyota huyo huenda akaonesha makali yake msimu huu.
Inaelezwa kuwa mchezaji, Aaron Ramsey ni kati ya wachezaji
waliobebeshwa lawama kubwa msimu uliopita kwenye kikosi cha Arsenal, baada ya kushindwa kupambana na
wachezaji nyota waliong’ara msimu huo.
Akichezesha nje ya nafasi yake ya upande wa mshambuliaji wa pembeni upande wa kulia ama kushoto, Ramsey alijaribu kila njia ili kuing’arisha timu yake lakini akashindwa kujijengea imani kwenye mioyo ya baadhi ya mashabiki wa timu hiyo ya Emirates.
Hata ilipofika karibu mwishoni mwa msimu huo, Ramsey kuhamishiwa kwenye nafasi ya katikati baada ya Jack Wilshere kuhangaika ili kujiweka sawa, lakini nyota huyo nako pia akajikuta akishindwa kufurukuta.
Lakini hata hivyo msimu huu Ramsey anaonekana huenda akazinduka, baada ya kuonekana shujaa kwenye baadhi ya mechi, jambo ambalo linawafanya mashabiki kuona kama mchezaji mpya aliyesajiliwa msimu huu.
Hadi sasa tayari ameshazifumania nyavu mara tatu na huku mchezaji bora wa mwezi wa klabu hiyo, Wilshere akionekana bado kupwaya, inaonekana kuwa huenda nyota huyo akawa muhimili wa sehemu ya kiungo kwenye kikosi hicho cha Arsene Wenger kwa mwaka huu.
4. Gary Cahill | Chelsea
Gary Cahill awali alikuwa akionekana bonge la mchezaji, baada ya
kutua kwenye klabu hiyo akitokea kwenye timu ya Bolton Wanderers kwa kitita cha pauni milioni.Kabla ya kutua kwenye klabu kubwa kama Arsenal na Tottenham, nazo zilikuwa zikimfukuzia nyota huyo wa timu ya Taifa ya England, lakini ilikuwa ni Chelsea ambayo ilifanikiwa kunasa saini ya nyota huyo.
Hata hivyo baada ya kucheza mechi 24 msimu uliopita hali ya wasiwasi ilianza kuwaingia mashabiki kutokana na kiwango chake alichokionesha.
Katika kipindi hicho alionekana kushindwa kuhimili mikikimikiki ya Ligi Kuu, huku akishindwa kukabiliana na wapinzani wao nyota hali ambayo iliisababishia timu hiyo kutolewa mapema kwenye michuano ya Klabu Bingwa Ulaya.
Lakini kwa sasa akiwa ameshachezeshwa kikosi cha kwanza mechi tatu za Ligi Kuu, ilizocheza Chelsea msimu huu, Cahill anaonekana yupo tayari kuzinduka, hususani baada ya kuendelea kukosekana, John Terry.
Akionekana yupo fiti zaidi na kujituma kwake msimu huu, Cahill anaonekana anaweza kuwa msaada msimu huu kwenye kikosi hicho cha kocha Jose Mourinho.
5. Shinji Kagawa | Manchester United
Shinji Kagawa alisaini Manchester United msimu uliopita kwa ada ambayo inaripotiwa kuwa ni ya pauni milioni 17.Nyota huyo alisajiliwa na klabu hiyo baada ya kuridhika na kiwango chake alichokionesha akiwa na timu ya Borussia Dortmund, inayokipiga kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani ya Bundesliga na akaonekana angeweza kukabiliana na hekaheka za Ligi Kuu ya England.
Hata hivyo, baada ya kutua kwenye kikosi hicho alionekana si lolote baada ya kushindwa kujihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza cha klabu hiyo ya Old Trafford.
Kukabiliwa na majeraha na vita ya kugombea namba na Wayne Rooney ilishuhudiwa akichezeshwa mechi 17 tu za Ligi Kuu msimu uliopita.
Lakini inaelezwa kuwa kwa mwaka huu anaonekana anaweza kuwa amebadilika, baada ya kufunga hat-trick dhidi ya Norwich City, mtanange uliopigwa kwenye Uwanja wa Old Trafford na idadi hiyo ambayo inamfanya afikishe mabao sita inadhihirisha wazi Kagawa huenda akatoa mchango mkubwa wa kupatikana mabao mengi, ukijumlisha pamoja na kipaji chake.
Mbali na hilo, inaelezwa pia endapo atakuwa na uhakika wa kucheza kila mechi, inaweza kushuhudiwa nyota huyo akinyakua tuzo ya mchezaji bora wa kulipwa wa mwaka akiwa katika kipindi chake cha miaka 24.
No comments:
Post a Comment