TIMU
nyingine 16 za Ligi ya Mabingwa zilionyeshana kazi juzi Jumatano na kuwepo na
matukio ya kushangaza kuliko yale ya Jumanne.
Chelsea
wakiwa na matumaini ya kuanza vizuri, wakiwa chini ya kocha wao, Jose Mourinho,
wakiwa nyumbani dhidi ya Basel, mambo
yalikuwa mabaya.
Pamoja
na Arsenal kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, lakini walikumbana na upinzani
mzito kutoka kwa wenyeji wao, Marseille.
Barcelona
waliwakaribisha Ajax katika Uwanja wa Camp Nou na hii ilikuwa ndio mechi bab
kubwa kwa usiku ule wa Jumatano.
Utamu
zaidi ulikuwa pale Lionel Messi, alipopiga ‘hat-trick’ wakati Barca wakiibuka
na ushindi wa mabao 4-0.
Kwa
sasa Messi amefikisha mabao 62 kwenye Ligi ya Mabingwa na kuwa mchezaji wa
kwanza kufunga zaidi ya ‘hat-trick’ katika ligi hiyo, huku akiwa ameifungia
klabu yake ya Barca ‘hat-trick’ 24.
Siku
moja kabla ya Messi kupiga ‘hat-trick’, mpinzani wake, Cristiano Ronaldo, na yeye
alipiga ‘hat-trick’ wakati Real Madrid wakiichapa Galatasaray mabao 6-1 katika
ligi hiyo ya mabingwa na kuonekana kama vile amejibu mapigo kwa mpinzani wake
huyo.
Baada
ya ‘hat-trick’ ya Ronaldo, baadhi ya wachambuzi wa soka walionekana kumkebehi
Messi na kusema hana kitu.
Lakini
kwa hat-trick hiyo ya Leo Messi, amedhihirisha kuwa alistahili kuwa mshindi wa
tuzo ya mchezaji bora wa dunia (Ballon d'Or) kwa mara ya nne.
Wachezaji
hao, wamekuwa na upinzani mkubwa uwanjani hata katika kinyang’anyiro cha tuzo za
Ballon d'Or na kila mara Messi ameonekana kuwa kidume.
Huenda
Messi, ameshawishiwa na ‘hat-trick’ ya Ronaldo, hivyo hakuna budi mambo ya
Ronaldo tumuachie Messi ashughulike nayo mwenyewe uwanjani.
Pamoja
na klabu hizo kunyakua mataji nane ya Ligi ya Europa na Ligi ya Mabingwa kwa pamoja,
Barcelona na Ajax hawajawahi kukutana kabla ya mechi ya juzi ya Kundi H kwenye
Uwanja wa Nou Camp.
Zaidi
ya yote, Messi alionyesha kiwango kikubwa kama msimu ule wa mwaka 2009 na 2011,
ambao waliibuka na mataji lukuki.
Ushindi
huo ulikuwa mahususi kwa Kocha wa Barca, Gerard Martino, ambaye atakwenda Argentina
kwenye mazishi ya baba yake.
“Ilikuwa
mechi ya aina yake. Inauma kwa kile kilichotokea, lakini wote tuko pamoja naye,”
alisema Messi, akimzungumzia kocha wake, Martino.
Ajax
walikuwa chini ya kiwango chao kile walichoonyesha mwaka 1995 waliponyakua taji
lao la nne la Ligi ya Mabingwa.
Bao
la kwanza la Messi lilikuwa la mpira wa adhabu, ambao aliupiga karibu na lango
la wapinzani na kugonga mwamba kabla ya kutinga wavuni.
Lile
la pili lilikuwa la aina yake, baada ya Messi kupokea pasi kutoka kwa kiungo Sergio
Busquets, akiwa upande wa kulia na kuingia nao ndani na kuachia shuti kwa mguu
wake wa kushoto na kuandika bao la pili kwa Barca.
Beki
wa kati wa Barca, Gerard Pique, naye alifunga kwa kichwa, akiunganisha mpira wa
krosi uliopigwa na Neymar kutoka upande wa kushoto.
Lakini,
Messi hakutaka kuwaachia nafasi wengine wang’ae, baada ya kupachika bao lake la
tatu na la nne kwa klabu yake, baada ya kupokea pasi ya Xavi, dakika ya 15
kabla ya mpira kumalizika.
Mambo
yalikuwa mabaya zaidi kwa Ajax, pale Kolbeinn Sigthorsson aliposhuhudia penalti
yake ikidakwa na mlinda mlango wa Barca, Victor Valdes, baada ya Javier
Mascherano, kumuangusha Thurani Serero.
Katika
mechi hizo za makundi, mechi nyingine ilikuwa ni ile ya AC Milan, ambao
waliepuka aibu ya kutoka sare na Celtic katika uwanja wao wa San Siro, baada ya
Emilio Izaguirre kujifunga mwenyewe na Sulley Muntari kuongeza bao jingine na Rossoneri
kuibuka na ushindi.
Mourinho,
alishangazwa na matokea ya klabu yake ya Chelsea, baada ya kupokea kichapo cha
mabao 2-1 dhidi ya FC Basle katika Uwanja wa Stamford Bridge, kwenye mchezo huo
wa Kundi E.
Wenyeji
walionekana kuongoza, baada ya nyota wa Brazil, Oscar, kuwafungia bao la
kwanza, akiitumia vizuri kazi nzuri ya David Luiz na Frank Lampard.
Oscar
alipata nafasi nyingine ambayo angeweza kuongeza bao la pili, lakini shuti lake
liligonga mwamba.
Nyota
wa Basel, Mohamed Salah, aliupitisha vizuri mpira jirani na Ashley Cole na
kutinga wavuni katika dakika ya 71, kabla ya Marco Streller kupiga bao jingine
la kichwa na Basel kupata ushindi wasioutarajia.
Mourinho,
alionekana kuwa mtulivu na kusema: “Sijashtuka. Huo ndio ukweli, wakati mwingine hupati ushindi. Kiukweli sina
furaha. Tumerudishwa nyuma katika harakati za kufuzu, lakini tumebakiza mechi tano
na tutamaliza tukiwa katika nafasi mbili za juu.”
Schalke
04 wanaliongoza kundi hilo, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Steaua
Bucharest.
Nyota
wa Japan, Atsuto Uchida na kiungo wa Ghana, Kevin-Prince Boateng na nyota wa
Ujerumani, Julien Draxler, ndio waliotingisha nyavu za Steaua Bucharest na
kuipa Schalke ushindi huo.
Mshindi
wa pili msimu uliopita, Borussia Dortmund, amekumbwa na majanga, baada ya
kuanza vibaya kwa kupokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Napoli, katika mchezo
wa Kundi la F, ambalo linajulikana kama Kundi la Kifo.
Ilikuwa
huzuni kwa Wajerumani hao, ambao mwishoni mwa wiki waliichapa Hamburg mabao
6-2, kufuatia kocha Jurgen Klopp na mlinda mlango Roman Weidenfeller wote kuonyeshwa
kadi nyekundu, baada ya Gonzalo Higuain
kufunga bao la kuongoza.
Lorenzo
Insigne, aliongeza bao la pili kwa Napoli, kabla ya bao la kujifunga mwenyewe
la Camilo Zuniga.
Arsenal
waliungana na Napoli kileleni mwa kundi hilo la kifo, baada ya kuibuka na
ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Marseille, katika Uwanja wa Stade Velodrome.
Kocha
wa Arsenal, Arsene Wenger, alisema bao la kwanza ndio lilikuwa msingi wa
ushindi.
“Nilijua
tangu matokeo yakiwa 0-0, baada ya nusu saa nilikuwa na uhakika kuwa timu itakayopata
bao la kwanza ndiyo itakayoibuka na ushindi,” alisema Wenger.
Winga
Theo Walcott, alifunga bao la kwanza kwa shuti kali, kabla ya Aaron Ramsey,
kuendelea kuonyesha kiwango chake kizuri kupachika bao la pili na la sita kwa
msimu huu.
Jordan
Ayew, alifunga bao la penalti dakika za majeruhi, baada ya Ramsey, kumuangusha
Jordan na Andre Ayew.
Atletico
Madrid walikuwa na usiku mzuri kwa kuwachapa wageni wao, Zenit St Petersburg
mabao 3-1.
Miranda,
alifunga bao la kwanza kabla ya nyota wa Brazil, Hulk kusawazisha.
Lakini,
mabao kutoka kwa Arda Turan na Leo yaliifanya Atletico kuongoza Kundi G, juu ya
Porto, ambao wameshinda bao 1-0 ndani ya Uwanja wa Austria Vienna, likifungwa
na Lucho Gonzalez.
No comments:
Post a Comment