* England inategemea nafasi ya timu kwenye ligi
* Hispania ni uwezo, nguvu ya timu
* Wingi wa mashabiki, historia vigezo Italia
STORI kubwa kwenye vyombo vya habari wiki hii, ni
kitendo cha klabu ya Yanga kupinga mechi zake kuonyeshwa na kituo cha
televisheni cha Azam.
Kila mtu amesema yake kuhusiana na sakata hilo, kuna
wanaoiponda Yanga na wale wanaoiunga mkono kwenye ishu nzima ya haki za
televisheni.
Pande zote mbili kwenye sakata hili zinahoja, kwa
sababu kila mtu anasema kile anachokiamini yeye kwa mtazamo wake.
Makala haya hayajalenga kuegemea upande wowote
katika sakata hili, lakini kwa sababu lengo la kila kinachofanyika ni kutaka
ligi ya Tanzania kuwa na ubora kama wa nchi za Ulaya, basi tumeona kuna umuhimu
wa kuangalia wenzetu wanafanya nini na kulinganisha na hali ilivyo kwenye
sakata hili.
Mkataba
wa Azam Tv
Dili la televisheni la Azam Tv ni la miaka mitatu,
ambalo thamani yake ni shilingi bilioni 5.56, huku wakitaka kuonyesha jumla ya
mechi 182 kati ya hizo 60 tu ndio moja kwa moja (live), nyingine zitakuwa
zilizorekodiwa.
Katika dili hili, Azam Tv watakuwa na haki ya
kuonyesha mechi nne za kila timu kwa msimu, huku wakitoa kiasi cha shilingi
milioni 100 kwa timu zote, lakini kiasi hicho kitapanda kadri miaka inavyosonga
mbele.
Asilimia 25 ya hizo milioni 100 itatolewa kwa klabu
kabla ya ligi kuanza na kipengele muhimu kuliko vyote ni kwamba, hakuna timu
itakayolipwa zaidi ya mwenzake.
Madai
ya Yanga
Katika kupinga michezo yao kuonyeshwa, Yanga
wamekuja na hoja tano, ambazo Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Yusuf Manji alizieleza
kwa wanahabari.
Hoja ya kwanza inakichwa cha Bodi ya Tanzania
Premier League, wanadai kwamba bodi iliyoko sasa ni ya mpito na haikuchaguliwa
kidemokrasia na haitakiwi kuingia mikataba ya muda mrefu wakati huu ikikaribia
kuondoka madarakani, pia haina mjumbe hata mmoja kutoka Yanga.
Hoja ya pili ya Yanga ni utaratibu
wa dunia nzima, humu wamesema hakuna sehemu yoyote duniani timu ikalazimishwa
kuachia haki zake za televisheni, huku pia wakipinga kugawana sawa mapato ya
televisheni na timu nyingine kwa kudai kwamba kipengele cha nafasi ya timu
kwenye Ligi lazima kiangaliwe na pia mkataba huo umekosa viwango (Premiums) na
kusisitiza hii itapoteza ushindani kwenye ligi.
Hoja ya tatu ya Yanga ni
kwamba, migogoro ya maslahi, humu wamedai kwamba Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya
Mpito ya TPL ni Mkurugenzi mwandamizi wa Makampuni ya Azam na kwa hivyo mazungumzo ya siri kati ya Bodi ya
TPL na Azam ni ya kutiliwa mashaka.
Pia wameeleza kwamba, Makampuni ya Azam yanashindana
kibiashara na makampuni mengi yakiwemo ya utengenezaji wa vinywaji baridi,
hivyo hili litahatarisha biashara na udhamini wa Yanga kutoka kwa makampuni mengine
yenye upinzani na Yanga. Pia wakadai kwamba Azam FC wanauadui wa kimichezo na
Yanga, wakitolea mfano sakata la Mrisho Ngassa kupelekwa Simba kwa mkopo.
Hoja ya nne ni kukosekana kwa uwazi, katika hili
walidai kwamba, mchakato mzima wa kurusha matangazo ya Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara ulifanywa kwa siri na hakushindanishwa, huku wakiongeza kwamba
hata Yanga ilipoomba kuupitia mkataba huo kisheria ilinyimwa.
Na la mwisho ni mazingatio ya kibiashara, wanadai
kwamba, Mahakama ya Kisheria ndiyo yenye haki ya kuamua mzozo wowote leseni na
siyo FIFA, lakini TPL wanasingizia ni FIFA, wanasema wahusika wote wanatakiwa
kuhusishwa kwenye mchakato huo kwa sababu una maslahi ya kibiashara. Pia
walizungumzia kuhusu kupungua kwa mapato ya mlangoni ambayo ni chanzo muhimu
cha mapato cha Yanga ambapo kila mchezo wanaweza kuingiza milioni 50 na zaidi,
ni zaidi ya milioni 8.2 ambazo zitapatikana katika mapato ya televisheni.
Baada ya kuona ofa ya Azam Tv na madai ya Yanga,
sasa tuangalie wenzetu walioendelea hali ikoje.
Hali
ilivyo England
England ndiyo nchi ambayo huvuna kiasi kikubwa cha
fedha kwenye suala zima la urushwaji wa mechi zake kwenye televisheni, na hivi
ndivyo mchakato mzima ulivyo.
Mkataba wa kurusha matangazo ya redio na televisheni
Ligi Kuu England, huuzwa kwa miaka mitatu mitatu na hufanywa kwa mfumo wa
mnada. Haki huuzwa katika mafungu sita na kila fungu linaonyesha mechi 23, na
hakuna televisheni moja ambayo hupewa haki ya kununua mafungu yote sita. Mafungu
hayo hupewa jina la A-F na yanatofautishwa na muda wa mechi kurushwa.
Ligi Kuu England huuza haki zake za televisheni kwa
ujumla wa timu zote na siyo timu moja moja kuuza haki zake, hii hutengeneza ‘balance’
ya mapato.
Kwenye Ligi Kuu England mapato ya haki za
televisheni, hugawanywa kwa wastani wa 50:25:25; Asilimia 50 hugawanywa sawa
miongoni mwa klabu, asilimia 25 hugawanywa kutokana na nafasi ambayo timu
itamaliza kwenye Ligi na asilimia 25 nyingine hutolewa kama gharama za kutumia
miundombinu ya klabu wakati wa kurusha matangazo. Wakati mapato yanayopatikana
nje ya Uingereza, hugawanywa sawa miongoni mwa klabu 20 za Ligi Kuu England.
Mkataba wa sasa wa haki za televisheni nchini
England, ni pauni bilioni 1.78 (shilingi trilioni 4.282), mkataba huo
unatarajiwa kukua na kufikia kiasi cha pauni bilioni 5 (shilingi trilioni
12.03) siku za usoni.
Mapato ya kuuza haki za televisheni ndani ya England,
yanaonyesha kwamba timu ambayo inamaliza juu kwenye ligi itapata fedha nyingi
kuliko ile ya chini, wakati yale ya nje ya England yanagawanywa sawa kwa timu
zote 20.
Mfano msimu uliopita, Manchester United waliokuwa
mabingwa wa Ligi Kuu England, waliingiza kiasi cha pauni milioni 13.4 (shilingi
bilioni 32.24) na Queens Park Rangers ilimaliza katika nafasi ya mwisho kwenye
Ligi ilipata pauni milioni 5.8 (shilingi bilioni 13.955).
Hali
ilivyo Ujerumani
Bundesliga wamesaini mkataba mpya wa kuonyesha mechi
zao siku za karibuni, mkataba huo utakuwa kati ya mwaka 2013 -2016 na unaanza
kufanya kazi rasmi msimu ujao.
Fedha za haki za televisheni kutoka ndani ya
Ujerumani, ni euro milioni 628 (shilingi trilioni 1.318) na nje ya Ujerumani ni
euro milioni 70 (shilingi bilioni 146.941) kwa msimu.
Mgawanyo wa fedha za haki za televisheni kwenye Bundesliga
kwa msimu, ni tofauti na nchi nyingine za Ulaya, huku kuna mfumo wa pointi
(Point System).
Asilimia 40 ya mapato yanagawanywa kulingana na
pointi za timu kwenye msimu uliopo (kwa sasa ni msimu wa 2013-14), na nafasi
kwenye ligi katika kila siku ya mechi inajumuishwa humu. Asilimia 30 inaangalia
msimu uliopita (2012-13), asilimia 20 msimu kabla ya uliopita (2011-12), na
asilimia 10 miaka mitatu iliyopita (2010-11).
Bingwa msimu wa 2010-11 anapewa pointi 36, mshindi
wa pili 35 mshindi wa tatu pointi 34. Msimu wa 2011-12 mshindi wa kwanza
anapata pointi 72, wa pili 70 na wa tatu 68, msimu wa 2012-13 mgawanyo wa
pointi kwa timu tatu za juu ni 108, 105 na 102. Unaweza kuona pointi hizo
zinazidishwa mara mbili.
Cha kuelewa hapa ni kwamba, pointi hizi zinatumika
kujua timu itakuwa nafasi ya ngapi wakati wa mgao wa mapato ya televisheni.
Timu yenye pointi nyingi itashika nafasi ya kwanza (msimu wa 2013-14) na
itapata euro 760,000 zaidi ya mshindi wa pili, tofauti hii itaendelea
kuongezeka mpaka kwa timu iliyoshika mkia.
Tofauti ya bingwa na aliyeshika mkia
mara mbili zaidi. Hali ilivyo sasa, Bayern watapata euro milioni 25.84 (shilingi
bilioni 54.242), Dortmund euro milioni 25.07 (shilingi bilioni 52.626) wakati
timu iliyoshika mkia Greuther Furth, ilipata euro milioni 12.92 (shilingi bilioni
27.121) kwa msimu ujao.
Pia kuna kiasi kidogo cha fedha kinatolewa kwa timu
kutokana na haki stahiki, hii inategemea idadi ya mechi zake ilivyoonyeshwa na
klabu zake.
Hali
ilivyo Hispania
Hispania sasa hivi wanajaribu kubadili mfumo wake
kutoka ule wa haki za televisheni kutawaliwa na Real Madrid na Barcelona, mpaka
ule wa angalau mgao sawa.
Mfano msimu uliopita, Real Madrid iliingiza euro
milioni 140 (shilingi bilioni 293.883) kwa kuuza haki zake za televisheni, timu
iliyowakaribia ni Barcelona ambao waliingiza euro milioni 134 (shilingi bilioni
281.288), wakati hali ikiwa hivyo kwa Barca na Madrid timu nyingine zimekuwa
zikipata kiasi kidogo sana mfano Granada walifanikiwa kupata euro milioni 12 (shilingi
bilioni 25.189).
Sasa hivi Serikali ya Hispania inaangalia uwezekano
wa kuanzisha sheria ambayo itazibana Barca na Madrid na kuuza kwa pamoja haki
zao za televisheni na kuziwezesha timu nyingine angalau kupambana nao.
Barcelona na Real Madrid wanaingiza mara 10 zaidi ya
timu nyingine 12 za La Liga, ni Atletico Madrid na Valencia ambazo angalau
wanakaribiana na timu hizo mbili, japo nao wameachwa mbali kiuhalisia.
Hali
ilivyo Italia
Serie A, Novemba mwaka jana waliingia mkataba mpya
wa televisheni ambao utadumu kati ya msimu wa 2012-13 hadi 2014-15, mkataba huo
unathamani ya euro milioni 840 (shilingi trilioni 1.763), katika dau hilo timu
zinazoshuka daraja zitapewa euro milioni 30 (shilingi bilioni 62.974) kwa ajili
ya kuwasaidia huko chini.
Tofauti na England ambapo hupanga mgawanyo mzima
mwisho wa msimu, Italia mgawanyo hufanywa kabla ya msimu kuanza hasa kwa
kuangalia taarifa za kihistoria.
Kuna vitu vitano vinaangaliwa wakati wa kugawanya
fedha za haki za televisheni na vitu hivyo ni pamoja na:-
Dau la pamoja (Dau Fixed Amount Element), ambalo
kila timu hupata pauni milioni 15.2 (shilingi bilioni 36.571).
Ishu ya pili ni Idadi ya mashabiki (Supporters Index
Element), hapa kuna asilimia 25 ya mapato yote, idadi hii hujulikana kupitia
utafiti uliofanywa na makampuni mbali mbali na kuna jumla ya mashabiki milioni
37.6 nchini Italia. Juventus ambao wanatajwa kuwa na mashabiki wengi zaidi
hufaidika hapa na hupata pauni milioni 45 (shilingi bilioni 108.272),
kulinganisha na Siena yenye mashabiki wachache hupata pauni milioni 1.2 (shilingi
bilioni 2.887).
Kitu cha tatu wanaangalia ni Idadi ya watu kwenye
mji timu inatoka (Town Population), kipengele hiki fedha hugawanywa kulingana
na idadi ya watu kwenye mji timu inatoka, hapa timu mbili za Turin (Torino na
Juventus), wanapata dau sawa. Wanaofaidika sana hapa ni Roma wanapata pauni
milioni 5 (shilingi bilioni 12.5), kulinganisha na Siena na Chievo wanaopata
pauni 300,000 (shilingi milioni 721.8).
Nafasi ya msimu uliopita (last season performance),
kuna dau ambalo hupangwa kutokana na nafasi ambayo timu ilimaliza msimu
uliopita, hapa ni asilimia tano tu ya pato lote ndiyo hutolewa.
Misimu mitano iliyopita (Last 5 seasons) hapa kuna
asilimia 15, mgao huu huangalia sana nafasi ambayo timu imemaliza kwenye misimu
mitano iliyopita, timu kubwa ndiyo zinafaidika sana na hili kwa sababu zina uhakika
wa kufanya vizuri kila msimu.
Sababu za Kihistoria (Historical Results Element),
asilimia 10 ya mgao wote huwekwa hapa, historia hiyo ni kuanzia mwaka 1946, kwa
mara nyingine Juventus na miamba ya Milan ndiyo inafaidika sana hapa kwa sababu
wamekuwa juu kwa muda mrefu sana na historia inawabeba sana wao.
Hitimisho
Ni ndoto ya kila
Mtanzania kuona siku moja Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inakuwa kama zile
za Ulaya na ili hili lifanikiwe ni lazima tufuate wanachokifanya kwa asilimia
kubwa hata kama tutafanya yetu.
Na kwa jinsi hali ya
mambo ilivyo kwenye nchi za wenzetu, hakuna hata nchi moja ambayo timu zote
zinapata mgao sawa, hivyo basi kwa kuangalia na wanachokisema Yanga, utagundua
kwamba kina mashiko kwa asilimia kubwa, haiwezekani timu ya mwisho kwenye ligi
ipate mgao sawa na bingwa, hivyo basi TPL na Azam TV hawanabudi kuangalia upya
mchakato mzima na kuja na mkataba bora ambao kila timu itaridhika nao.
No comments:
Post a Comment