LICHA ya kukamilisha usajili wake kwa ajili ya msimu ujao wa
Ligi Kuu ya Soka ya Vodacom Tanzania Bara, klabu ya Simba huenda ikajikuta na
pengo kubwa mwanzoni mwa msimu, baada ya wachezaji wake wanne muhimu,
kutarajiwa kuondoka kwenye kikosi hicho kwenda nchini Uingereza.
Mfadhili wa Simba, Rahma Al Kharusi ‘Malkia wa Nyuki’, amefanikiwa kuishawishi timu ya
Sunderland ya Uingereza kuwafanyia majaribio wachezaji wake wanne, akiwemo kipa
namba moja wa timu hiyo kwa sasa, Abel Dhaira.
Hatua hiyo imekuja baada ya Malkia wa nyuki
kufanya mazungumzo na mmiliki wa Sunderland, Ellis Short hivi karibuni.
Habari za ndani zilizoifikia LENZI YA MICHEZO kutoka kwenye Kamati ya Utendaji ya timu hiyo, zilisema kuwa mbali na Dhaira,
wachezaji wengine watatu wa Simba watapata nafasi hiyo.
Chanzo hicho kilisema kuwa wachezaji hao
watafanya majaribio katika academia ya timu hiyo kwa muda wa wiki mbili.
“Kama watafuzu majaribio yao, basi watapata nafasi ya
kucheza ligi ya vijana ya nchi hiyo na jinsi watakavyoendelea baadaye itakuwa
nafasi ya kupata nafasi ya kucheza ligi kuu,” alisema.
Chanzo hicho kiliwataja wengine kuwa ni beki
kiraka ambaye kwa sasa yupo kwenye majaribio nchini Uholanzi, Shomari Kapombe,
Ramadhani Singano na mmoja ambaye kamati haijaamua.
Chanzo hicho kilisema kuwa wachezaji hao wametakiwa
kuwasilisha wasifu wao (CV), pamoja na nyaraka nyingine muhimu ili kuanza
taratibu za safari.
“Wachezaji hao wataondoka hivi karibuni kwa kuwa wameanza
utaratibu wa kuwasilisha wasifu wao, huku Simba ikifuatilia safari hiyo,”
alisema.
Awali winga Mrisho Ngassa na Shomari Kapombe walichaguliwa
kwenda kwenye majaribio katika timu hiyo ya Sunderland, ila safari hiyo
haikuweza kutimia.
No comments:
Post a Comment