KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa timu ya Yanga, Nurdin
Bakari na wenzake watatu waliokuwa wanachezea Ligi Kuu msimu uliopita,
wamesajiliwa na Rhino Rangers kwa ajili ya msimu wa 2013/14.
Akizungumza na LENZI YA MICHEZO, Kocha Mkuu mpya wa Rhino
Rangers, Sebastian Nkoma alisema kuwa Nurdin alisajiliwa wiki iliyopita pamoja
na wachezaji wengine wakongwe wazoefu wa ligi kuu.
Aliwataja wachezaji wengine waliosajiliwa pamoja na Nurdin
kuwa ni mabeki, Ladislaus Mbogo aliyeachwa na Yanga, Laban Kambole na Salum
Kamane kutoka Kagera Sugar.
Kocha huyo ambaye amerithi mikoba ya Renatus Shija
aliyetimuliwa alisema uongozi wa timu hiyo mpaka sasa umekamilisha usajili wa
wachezaji 27 wengi wakiwa ni wageni katika michuano ya Ligi Kuu huku wazoefu
wakiwa ni hao wanne tu.
“Jana (juzi), tumefunga rasmi usajili wetu kwa ajili ya ligi
kuu msimu huu, tuna imani kikosi hicho kitaweza kuhimili vishindo na kuleta
ushindani katika ligi hiyo,” alisema.
Nkoma alisema kwa sasa wachezaji wote akiwemo Nurdin,
wamesharipoti kambini kujiandaa na ligi hiyo inayotarajiwa kuanza Agosti 24
mwaka huu, ambapo Rhino imepangwa kuanza na Simba katika Uwanja wa Ally Hassan
Mwinyi, mjini Tabora.
No comments:
Post a Comment