SERENGETI BOYS 'BYE BYE' KOMBE LA DUNIA
TIMU ya Taifa ya vijana ya soka chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imeaga fainali za Kombe la Dunia baada ya kufungwa mabao 3-1 na Ireland kwenye Uwanja wa Aspire Zone nchini Qatar.
Mchezo huo ulikuwa na kasi na mashambulizi mengi na mabao yote yalifungwa kipindi cha kwanza.
Ireland ilipata bao la kuongoza dakika ya sita lililofungwa na Cillian Murphy akimalizia pasi ya Ryan Sheridan na dakika ya 18 Luqman Mbalasalu aliisawazishia Serengeti Boys na kurejesha matumaini kwa Tanzania.
Dakika ya 26 Cillian Murphy wa Ireland alirejea tena nyavuni na kufunga bao la pili dakika ya 30–31, Desmond Armstrong alifunga bao la tatu na kupunguza kasi ya Serengeti Boys.
Dakika ya 42 teknolojia ya vikure iliokoa jahazi la Serengeti Boys kwa kufuta penalti iliyokuwa imeamriwa kwenda langoni mwao.
Kipindi cha kwanza Serengeti ilitawala umiliki wa mpira kwa asilimia 53 na kukamilisha pasi sahihi 218 (asilimia 79), hata hivyo umiliki huo haukuleta madhara makubwa langoni mwa wapinzani, ukilinganisha na Ireland iliyocheza kwa kasi inapopata mpira. Ireland ilitengeneza mashambulizi ya hatari 26 dhidi ya 18 ya Tanzania, huku ikipiga mashuti manane yaliyolenga lango ikilinganishwa na manne ya Tanzania katika kipindi cha kwanza.
Benchi la ufundi la Serengeti Boys lilifanya mabadiliko matatu ya haraka mwanzoni mwa kipindi cha pili kwa kuwaingiza Faraji Kayanda, Bashiri Kibaila na Abubakar Othman, kisha kuongeza nguvu kupitia Dismas Athanasi (dakika ya 64) na Juma Sagwe (dakika ya 73) na kusaidia kuzuia Ireland isiongeze mabao zaidi lakini ngome ya Ireland ilisimama imara na kutoruhusu bao lolote hadi mwisho.
Kipigo hicho kimehitimisha safari ya Serengeti Boys katika hatua ya makundi ikiwa na pointi moja iliyoipata kwenye sare ya 2-2 dhidi ya Costa Rica (baada ya pia kufungwa 1-0 na Brazil).
Jamhuri ya Ireland imefikisha pointi sita na kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele katika hatua ya mtoano pamoja na Brazil.

Post a Comment