RAIS SAMIA AAPISHA VIONGOZI, AMTAKA DK RIOBA KUIMARISHA MAWASILIANO YA SERIKALI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtaka Mkurugenzi wa Idara ya Habari–Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Ayub Rioba Chacha, kuimarisha mawasiliano ya Serikali, na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa za mafanikio na utekelezaji wa mipango ya Serikali kwa wakati na kwa usahihi.
Aidha amewataka viongozi na watendaji katika ngazi za mikoa, wilaya na halmashauri nchini kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wanaowaongoza katika maeneo yao.
Rais Dkt. Samia ametoa amaagizo hayo tarehe 27 Novemba, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uapisho wa viongozi aliowateua hivi karibuni.
“Niwapongeze (wote) mlioapa leo, lakini hongera isiwaingie vichwani. Natarajia kuona kazi ikifanyika,” amesema Rais Dkt. Samia.
Pia amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kote nchini kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma ili zitumikekwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo itakayowanufaisha wananchi.
“Pesa hizi ni kwa ajili ya wananchi, si kwa ajili yetu,” amesema Rais Dkt. Samia,akisisitiza matumizi yanayofaa ya rasilimali za umma ili zilete manufaa kwa wananchi kupitia huduma na miradi iliyokusudiwa.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameeleza kwamba mabadiliko ya muundo yaliyofanyika kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Mifugo na Uvuvi yanalenga kuongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi.
Rais Dkt. Samia ameitaka Wizara mpya ya Mifugo kufufua mashamba ya mifugo ya Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi, ili kuongeza uzalishaji na kufungua fursa za ufugaji na ajira kwa vijana kupitia programu ya Kesho iliyo Bora (Building a Better Tomorrow).
Aidha, ameitaka Wizara hiyo kudhibiti dawa bandia na zisizokidhi viwango zinazouzwa kwa wafugaji.
Vilevile, ameitaka Wizara mpya ya Uvuvi kuhakikisha inafanya mageuzi ya kisera na kitaasisi kwa lengo la kuongeza tija ya shughuli za uvuvi, hususan uvuvi wa Bahari Kuu, uendeshaji wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa, pamoja na kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi.
Rais Dkt. Samia ameitaka Wizara ya Kilimo kuchukua hatua dhidi ya mbolea bandia, kuzuia pembejeo za ruzuku kuuzwa nje ya mfumo na kushughulikia vyama vya ushirika vinavyowakandamiza wakulima.
Halikadhalika, ameitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuimarisha kliniki za ardhi, kusimamia uadilifu wa maafisa ardhi, na kuhakikisha kero na migogoro ya ardhi inatatuliwa.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA), Mhandisi Gilbert Godfried Mwoga,kusimamia ujenzi wa barabara zenye kukidhi viwango, kuhimili mabadiliko ya hali ya hewa, na zinazodumu muda mrefu ili kupunguza gharama za matengenezo na kurahisisha wananchi kuzifikia huduma muhimu, ikiwemo za afya.












Post a Comment