TPA YANG’ARA KATIKA TUZO ZA NBAA KWA UBORA WA TAARIFA ZA FEDHA



Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeendelea kuonesha ubora katika usimamizi wa fedha na uwajibikaji baada ya kutwaa tuzo ya” Best Presented Financial Statements” na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), ikiwa ni kutambua ubora wa maandalizi na uwasilishaji wa taarifa zake za fedha kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu vya uhasibu.

Mkurugenzi Mtendaji, wa NBAA, CPA Prof. Siasa Issa Mzenzi amesema tuzo hizi ni kielelezo cha juhudi za taasisi hizi katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha, utunzaji wa kumbukumbu za kihasibu na kuhakikisha taarifa za fedha zinaandaliwa kwa usahihi, uwazi na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

Mafanikio hayo yanaenda sambamba na rekodi ya TPA kupata hati safi ya ukaguzi wa hesabu kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), jambo linaloonesha dhamira ya taasisi katika kuzingatia misingi ya uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa rasilimali za umma.

Hivi karibuni wakati wa sherehe za utoaji gawio kwa taassi za umm, TPA imeendelea kuongoza miongoni mwa taasisi za umma katika utoaji wa gawio kwa Serikali kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo. Mafanikio hayo yanaakisi uwezo wa taasisi katika kusimamia shughuli zake kwa ufanisi, kukuza mapato na kuchangia katika juhudi za Serikali za kuimarisha maendeleo ya taifa.






Akipokea tuzo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Mbarikiwa Masinga amesema kwamba mafanikio haya yanatokana na kuimarishwa kwa mifumo ya ndani ya udhibiti, usimamizi wa mapato na matumizi, nidhamu ya matumizi ya fedha pamoja na ushirikiano na uwajibikaji wa watumishi katika ngazi mbalimbali za taasisi.

Bw. Masinga amesisitiza kwamba mafanikio haya yanaendelea kujenga na kuimarisha imani ya wananchi kwa TPA, yakionesha dhamira ya taasisi katika kusimamia rasilimali za umma kwa uadilifu, uwazi na weledi.

"TPA inaendelea kujizatiti katika kuboresha mifumo yake ya kiutendaji na kifedha ili kuhakikisha inaongeza tija, inaimarisha uwajibikaji na kuchangia kwa ufanisi zaidi katika ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia sekta ya bandari" amesema.

Jumla ya taasisi 139 zilishirikia katika tuzo hizo mwaka huu, ukilinganisha na taasisi 86 zilizoshiriki mwaka jana.


No comments