JAMII YAASWA KUTOVUMILIA VITENDO VYA UKATILI
Naibu
Waziri Katimba ameeleza kuwa Serikali imekuwa ikitekeleza mipango na kampeni
mbalimbali za kupambana na ukatili huo, ikiwemo Kampeni ya Msaada wa Kisheria
ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) pamoja na Mpango Kazi wa Taifa wa
Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto Awamu ya Pili wa mwaka 2024/25
hadi 2028/29.
Ameongeza
kuwa afua zingine zinazotekelezwa na Serikali ni pamoja na Kampeni ya Kitaifa
ya kulinda watoto dhidi ya ukatili wa mtandaoni, uanzishwaji wa madawati ya
jinsia katika Jeshi la Polisi, vyuo vikuu na vya kati, pamoja na maeneo ya umma
ili kutoa huduma kwa wahanga wa ukatili. Hatua hizo zote zinalenga kuunga mkono
utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 kwa kuhakikisha mtaji watu unalindwa dhidi ya
ukatili.
Akitoa
salamu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,
Eliakim Chacha Maswi amebainisha kuwa vita dhidi ya ukatili inashirikisha wadau
mbalimbali ili kuongeza nguvu ya kutokomeza janga hilo kupitia usimamizi wa
Jamii Ajenda 2050 inayolenga kufikia familia na taifa imara.
Naye
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Daktari Khatibu Kazungu, amesema mkoa huo
umeifanya vita dhidi ya ukatili kuwa ajenda ya mkoa kwa kushirikiana na
wataalamu na wadau kutoa elimu, kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa, na kujenga
ushirikiano baina ya taasisi husika.
Wakati
huo huo, Mratibu wa Taasisi ya WILDAF, Wakili Anna Kulaya, amethibitisha
kujitolea kwa wadau mbalimbali katika kuhakikisha vitendo vya ukatili
vinatokokomezwa kupitia maadhimisho haya na majukwaa mengine.
Maadhimisho
ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia Kitaifa kwa mwaka 2026 yanaadhimishwa
kuanzia tarehe 25 Novemba hadi 10 Desemba 2026 yakiongozwa na kaulimbiu:
"Tuungane Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto: Jenga Taifa
Imara Lenye Haki na Usawa Kuelekea Dira 2050."










Post a Comment