CHAKULA CHA USIKU CHA NBC CHAPELEKA SALAMU UJENZI WA UCHUMI
BENKI ya Taifa ya Biashara NBC imesisitiza dhamira yake ya kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii nchini kwa kuendelea kuwekeza katika suluhisho za kifedha na kiteknolojia, ubia wa kimkakati pamoja na mipango ya uwajibikaji kwa jamii inayolenga kuunga mkono maendeleo ya sekta hiyo.
Dhamira hiyo ilisisitizwa na Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa na Serikali wa NBC, Elvis Ndunguru wakati wa hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake wakubwa kutoka kampuni na taasisi mbalimbali jijini Arusha.
Hafla hiyo, iliyowakutanisha viongozi na maofisa wa NBC pamoja na wawakilishi wa kampuni na taasisi mbalimbali, ililenga kuimarisha uhusiano kati ya benki na wateja wake, kubadilishana mawazo kuhusu fursa za biashara, kutambulisha huduma na suluhisho mpya za kifedha, pamoja na kupata mrejesho kuhusu namna NBC inavyoweza kuendelea kuboresha huduma zake kulingana na mahitaji ya wateja.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ndunguru alisema matukio kama hayo ni sehemu ya mkakati wa benki wa kuwa karibu na wateja wake, kuwaeleza maendeleo katika huduma za kifedha na kidijiti, pamoja na kuunda mazingira yanayowezesha wateja kubadilishana taarifa na fursa za biashara.
Alitaja baadhi ya maeneo ambayo NBC imeendelea kuboresha kupitia teknolojia kuwa ni mifumo ya ukusanyaji wa mapato na malipo ya serikali, ikiwemo GePG na MUSE, pamoja na suluhisho za ukusanyaji wa malipo kwa taasisi mbalimbali, zikiwemo Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro NCAA.
Arusha ni mkoa wa kimkakati katika utekelezaji wa ajenda yetu ya kuhudumia sekta ya utalii, na tutaendelea kuboresha na kuwekeza katika fursa mbalimbali, hususani katika maeneo ya utalii, sambamba na sekta nyingine zenye mchango mkubwa katika uchumi kama kilimo na ufugaji, alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa NBC Tawi la Arusha, Mukiza Mboneko alisema NBC inatoa huduma za mikopo kwa ajili ya ununuzi wa magari ya kubebea watalii, ujenzi na uendelezaji wa kambi za utalii, hoteli pamoja na mitaji ya biashara kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao ndani ya mnyororo wa thamani wa sekta ya utalii.
Pia, tuna mifumo ya malipo iliyounganishwa na TANAPA na Ngorongoro, inayowawezesha wadau kufanya malipo mbalimbali, ikiwemo ada za hifadhi, kwa urahisi zaidi, alisema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania TAWIRI, Dk Ernest Mjingo alisema huduma za kisasa za kifedha, hususani mifumo ya kidijiti zimeendelea kuwa muhimu kwa taasisi na wafanyabiashara katika kurahisisha miamala na ukusanyaji wa mapato.
Post a Comment