Kadogosa asifu utekelezaji wa miradi ya kimkakati
WAZIRI wa Ujenzi, Masanja Kadogosa amesema utekelezaji wa miradi ya kimkakati ni ishara ya uongozi imara unaolenga kuleta matokeo na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
Kadogosa alisema hayo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Jangwani mkoani Dar es Salaam juzi. Alisema Daraja la Jangwani ni miongoni mwa ahadi zilizotolewa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni.
“Rais wakati anafungua kampeni Kawe, katika vitu alivyozungumza na akashangiliwa sana ni pale alipozungumzia ujenzi wa daraja hili la Jangwani ambalo tunaliona,” alisema Kadogosa.
Aliipongeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) na mkandarasi kwa hatua iliyofikiwa na kutaka ukamilike ifikapo mwisho wa mwaka 2027.
Kadogosa alisema serikali inaendelea kuchukua hatua za kujiandaa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua kwa kuweka makalavati, madaraja ya muda na vifaa vingine muhimu ili kuhakikisha barabara kuu haziathiriwi na mvua. Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo alisema Daraja la Jangwani lina umuhimu katika shughuli za kitaifa, kisiasa, kidini na kijamii.
Mpogolo alisema kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kutasaidia kupunguza changamoto hizo, kuboresha mazingira na kurahisisha usafiri kwa wananchi.
Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal aliipongeza serikali kwa kuwekeza katika eneo hilo na akamshukuru Rais Dk Samia kwa kulipa kipaumbele Daraja la Jangwani. Awali, Meneja wa ujenzi wa mradi huo, Leonard Ngayungi alisema ujenzi umefikia asilimia 43 na unahusisha ujenzi wa daraja na miundombinu ya watembea kwa miguu.

Post a Comment