WANAFUNZI 150 WA SAMIA SCHOLARSHIP KUNUFAIKA NA UFADHILI WA MASOMO ALGERIA
Wanafunzi 150 wa Kitanzania wanatarajiwa kwenda kusoma vyuo vikuu nchini Algeria kupitia ufadhili uliotolewa na nchi hiyo, ikiwa ni sehemu ya wanafunzi 1,000 waliopata ufadhili wa Samia Scholarship kwa masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM).
Akizungumzia mpango huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alieleza kuwa serikali ya Algeria italipia ada zote za masomo, wakati Tanzania kupitia mpango wa Samia Scholarship itagharamia matumizi ya maisha ya wanafunzi hao.
Alisema nafasi hizo zitatolewa kwa kuzingatia ufaulu mzuri kwa kipaumbele zaidi kwa wanafunzi kutoka familia zenye kipato cha chini, huku serikali ikitakiwa kuwasilisha majina hayo kabla ya Septemba 15 ili kutoa nafasi ya maandalizi ya awali.
Profesa Mkenda alibainisha kuwa mchakato wa kuwapata wanafunzi hao umeanza baada ya kupunguza idadi ya awali kufuatia wanafunzi 10 kuchaguliwa kwenda Chuo Kikuu cha RUDN nchini Urusi na wengine 15 waliofanya vizuri zaidi katika michepuo maalum, na hivyo kufungua milango kwa wanafunzi 150 bora kutoka kundi lililobaki, wakiwemo wanafunzi wa mchepuo wa PCB.
Alifafanua kuwa majina ya wanufaika yatawekwa kwenye tovuti ya wizara na watahusika kupigiwa simu ili kupata maelekezo ya maombi na kusaidiwa upatikanaji wa hati za kusafiria, ambapo watakaoteuliwa watatakiwa kutumia mwaka mmoja kusoma lugha ya Kifaransa kabla ya kuanza masomo yao rasmi, huku akisisitiza kuwa nafasi hiyo ni hiari na ikitokea mwanafunzi amekataa atachukuliwa anayefuatia kwenye orodha ya ufaulu.
Alihitimisha kwa kusisitiza kuwa serikali itaendelea kutafuta fursa za masomo ya sayansi nje ya nchi ili kuwawezesha watoto wa wakulima na wafugaji kupata elimu ya juu na kuchangia maendeleo ya taifa.

Post a Comment