Mbunge abeba tofali kusaidia ujenzi wa shule
Mbunge wa Tunduru Kusini, Mhandisi Fadhili Chilombe ameungana na wananchi wa Kijiji cha Mkaleka kilichopo Wilaya ya Tunduru katika mradi wa ujenzi wa madarasa manne kwa lengo la kutatua changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya elimu.
Ujenzi wa mradi huo umeanza baada ya mbunge katika awamu ya kwanza kuchangia mifuko 100 ya saruji iliyosaidia wananchi kufyatua tofali na kuanza ujenzi.
Uenzi huo kwa sasa upo hatua ya madirisha, huku kiongozi huyo akiongeza ahadi ya kutoa mifuko mingine ya ziada ili kuhakikisha miundombinu hiyo inakamilika kwa wakati .
Akizungumzia katika mradi huo baada ya kushiriki kusogeza matofali kwa wajenzi, Mhandisi Chilombe alieleza kuguswa na kasi kubwa na jitihada zilizoonyeshwa na wananchi wa Mkaleka katika matumizi ya rasilimali zilizotolewa, hali iliyomshawishi kuongeza mpango wa awali wa kujenga madarasa mawili hadi kufikia madarasa manne kwa kuongeza mifuko mingine 300 ya saruji.
Mtendaji wa Kata ya Misechela, Said Issa Sapanga, alithibitisha kuwepo kwa changamoto kubwa ya watoto kulazimika kutembea umbali wa kilomita tisa hadi kumi kwenda Shule ya Msingi Misechela, hali iliyokuwa ikihatarisha usalama wao na kuathiri mahudhurio yao.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tunduru, Abdallah Mtila, aliwapongeza wananchi hao kwa moyo wa kujitolea na kasi ya utekelezaji iliyofikia viwango vya juu.
Mbali na elimu, mbunge hametoa ahadi za kusaidia sekta ya afya kupitia ujenzi wa zahanati katika Kijiji cha Misechela.



Post a Comment