KIKWETE AWATAKA WANAUME KUPIMA TEZI DUME MAPEMA
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
amewataka wanaume kujenga utamaduni wa kupima afya ya tezi dume mara kwa mara,
akisema uchunguzi wa mapema huongeza uwezekano wa kupata matibabu kwa wakati
kabla saratani haijasambaa.
Dkt. Kikwete ametoa wito huo jijini Dar es Salaam alipokuwa
mgeni rasmi katika maadhimisho ya Mwezi wa Uelewa wa Saratani ya Tezi Dume
yaliyofanyika katika Hospitali ya Kairuki, Mikocheni.
Katika maadhimisho hayo, Dkt. Kikwete alitembelea mtambo wa
kisasa wa High Intensity Focused Ultrasound (HIFU), unaotumika kutibu baadhi ya
uvimbe, ikiwamo saratani ya tezi dume kwa wagonjwa wanaostahili, bila kufanyiwa
upasuaji wa kawaida. Teknolojia hiyo hutumia mawimbi ya sauti yenye nguvu
kuelekeza joto katika eneo lenye uvimbe.
Akizungumza kuhusu uzoefu wake binafsi, Dkt. Kikwete alisema
alipogundulika mapema kuwa na dalili za saratani ya tezi dume mwaka 2014,
aliamua kufanyiwa uchunguzi wa kina nchini Marekani. Vipimo vilichukuliwa na
kuthibitisha kuwa saratani ilikuwa katika hatua za awali, hali iliyomwezesha
kuchukua hatua za matibabu mapema.
“Walichukua sampuli 14 na katika sampuli mbili wakaona
dalili za saratani. Madaktari wakaniambia kuwa ilikuwa inaanza na kwamba
ingeweza kutibika,” alisema.
Alisema alikubali kufanyiwa upasuaji wa kuondoa tezi dume
ili kuzuia saratani hiyo isisambae katika sehemu nyingine za mwili, na kwamba
tangu wakati huo ameendelea kuwa na afya njema.
“Baada ya kufanyiwa upasuaji nilijenga utaratibu wa kupima
afya yangu mara kwa mara. Kwa sasa afya yangu ni njema kabisa; ndiyo maana mtu
akisema ninaumwa, nacheka tu, kwa sababu ninaifahamu afya yangu,” alisema.




Post a Comment