MOTSEPE AKUBALI TANZANIA IPO TAYARI KWA AFCON 2027

 


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba, amelihakikishia Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) kwamba Tanzania ipo tayari kwa uenyeji wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yanayotarajiwa kuandaliwa na Tanzania kwa ushirikiano na mataifa ya Kenya na Uganda kuanzia Juni 19 mpaka Julai 17, 2027.

Dkt. Mwigulu ametoa hakikisho hilo Alhamisi, Septemba 17, 2026 kwa Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe, katika Ofisi Ndogo za Waziri Mkuu, Magogoni - Dar es Salaam, ambapo Waziri Mkuu amemwambia Dkt. Motsepe na ujumbe wake kutoka CAF kwamba maandalizi kwa upande wa Tanzania yanaendelea vizuri. 

"Tupo tayari, sio kwamba tumefurahi tu, tumefurahi na tupo tayari kuwa wenyeji, kuanzia sisi Serikali, mamlaka za soka na hata mashabiki, tupo tayari kwa mashindano haya," amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu katika mazungumzo yake ameongeza kusema anafahamu lengo mahsusi la ziara ya Dkt Motsepe ni kujionea na kukagua maandalizi ya mwisho na yeye kama Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, akifanya kazi bega kwa bega na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, wamekuwa wakifanya vikao na kutembelea miradi anasema Tanzania ipo vizuri.





"Tumekuwa tukipata mikakati ya namna tutahakikisha tunafanikisha maandalizi kama ilivyokusudiwa. Hivyo ninawahakikishia kwamba tumejizatiti kuhakikisha maandalizi yote yanakamilika ndani ya muda uliopangwa. Tumewaelekeza wasimamizi, wakandarasi na wote wanaohusika na utekelezaji wa miradi kufanya kazi usiku na mchana na kuhakikisha tupo ndani ya muda uliokusudiwa," amesisitiza Waziri Mkuu.

Dkt. Mwigulu amesema ni kiu ya Serikali kuona mashindano hayo yanafanyika, huku yakiwa ni miongoni mwa mashindano yaliyoandaliwa kwa viwango vya juu.

"Leo nilikuwa Arusha nimepata mrejesho wa ujenzi wa uwanja wa Arusha na miundombinu mingine, tupo hatua nzuri. Pia nimekuwa nikitembelea miundombinu ya hapa Dar es Salaam, hasa uwanja wa Benjamin Mkapa na miundombinu mingine."

"Tunawahakikishia, kufikia Disemba tutakuwa tumemaliza maandalizi. Njoeni muone baada ya Disemba, mtajionea kuwa kila kitu mlichoahidiwa hapa kimekamilika," amesisitiza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amesisitiza kuwa utayari wa Tanzania haupo katika kuandaa mashindano pekee, bali pia maandalizi ya uhakika ya timu ya taifa ili ikafanye vizuri kwenye mashindano hayo badala ya kuwa timu shiriki tu.

"Tunaandaa timu yetu, tunataka kuwa na Tshabalala wetu, kama alivyofanya Tshabalala wakati wa Kombe la Dunia (mwaka 2010) nchini Afrika Kusini, na sisi tunamuandaa Tshabalala wa kwetu. Na tuna mashabiki wazuri hapa kwetu, hivyo tunaiandaa vizuri timu yetu ili iendelee kuwa bora na kudhihirisha kuwa mwenyeji naye yupo tayari, kama ulivyoshuhudia kule Morocco timu yetu imeimarika," ameongeza Dkt. Mwigulu.

Kwa upande wake, Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe amesema anaamini mashindano hayo yatafanyika kama yalivyopangwa kwani mataifa yote yamefanya kazi nzuri ya maandalizi mpaka sasa.

"Uganda imefanya kazi nzuri, Kenya imefanya kazi nzuri pia, Tanzania imefanya kazi nzuri sana, Tanzania chini ya usimamizi wako imefanya kazi nzuri sana, na ninajivunia kazi ambayo Tanzania imefanya."

"Leo vyombo vya habari vilikuwa vinaniuliza ni lini utasema umefurahishwa na maandalizi, nikawaambia leo nimefurahi sana," ameongeza Dkt. Motsepe.

Pamoja na ujumbe wa Dkt. Motsepe kutoka CAF, pia kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa, Neema Msitha pamoja na wawakilishi wa kamati ndogo ya ndani ya maandalizi ya mashindano AFCON.

No comments