DC MPOGOLO AWASHUKIA WANAOISHI MABONDENI

 



MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi, hususani mabondeni na kwenye mikondo ya maji, kuhama mara moja na kutafuta maeneo salama ili kuepusha maafa yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha.

 Mpogolo alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake katika eneo la Viwege ambapo alizungumza na wananchi wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuwaeleza umuhimu wa kuchukua tahadhari mapema, hasa kipindi hiki ambapo inatarajiwa kuwapo kwa mvua kubwa za El Nino.

 “Mnafahamu kuwa maeneo haya mliopo hayaruhusiwi kuishi. Sasa ni vizuri kipindi hiki ambacho mvua hazijaanza mtafute mahali salama ili kuepusha maafa yanayoweza kutokea mvua zikianza,” alisema. 

Mpogolo pia amemuelekeza Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Ilala kuhakikisha mitaro na mabonde yanasafishwa ili kurahisisha upitishaji wa maji na kupunguza hatari ya mafuriko. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya alisema halmashauri hiyo inajiandaa kukabiliana na athari za mvua zinazotarajiwa. 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imeendelea kutoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa mvua za El Nino, na wananchi wakihimizwa kuchukua tahadhari, ikiwemo kuhama katika maeneo ya mabondeni na maeneo mengine hatarishi. 

Katika ziara hiyo, Mpogolo aliambatana na Mkurugenzi wa Jiji, Mabelya na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Selemani na walitembelea maeneo ya Viwege na Mbondole, Kata ya Majohe, kwa lengo la kutathmini hali ya mazingira na kuchukua hatua za kuimarisha usalama wa wananchi.


No comments