FAINI YA HADI SHMILIONI MOJA KWA YEYOTE ATAKAYECHAFUA JIJI LA DAR ES SALAAM


Yeyote atakayebainika kutupa takataka ovyo au kutiririsha maji holela ndani ya Jiji la Dar es Salaam sasa atakabiliwa na faini ya papo hapo kuanzia shilingi laki tatu hadi shilingi milioni moja au kifungo cha miezi 12 hadi 24.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo,kama sehemu ya mkakati mpya wa Halmashauri ya Jiji kusimamia Sheria ya Usafi wa Mazingira ya mwaka 2024 ili kutekeleza agizo maalum la Rais Dk Samia Suluhu Hassan la kufanya jiji hilo kuwa safi na salama. 

“Atakayekutwa anatupa uchafu hovyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Adhabu ni faini ya kuanzia shilingi laki tatu hadi milioni moja au kifungo cha miezi 12 hadi 24. Kila mmoja anatakiwa kutambua wajibu wake na kuacha mara moja tabia ya kutupa uchafu hovyo,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alitoa onyo leo, Septemba 19, 2026, baada ya kuhitimisha zoezi la usafi wa mazingira jijini, amesema sheria hiyo, Kifungu cha 41 cha Sheria Ndogo ya Afya, Usafi na Usimamizi wa Mazingira ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ya Mwaka 2024 (GN Na. 1011), itaanza kutekelezwa kikamilifu ili kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa safi, salama na yenye mazingira bora. 

Amesema Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi, lakini hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaotupa taka hovyo, kutiririsha maji au kufanya vitendo vingine vinavyokiuka sheria za usafi na mazingira.

Mpogolo amesema utekelezaji huo haulengi adhabu pekee, bali kujenga nidhamu, uwajibikaji na utamaduni wa usafi. Halmashauri pia itaendelea kuweka maeneo na vifaa vya kuhifadhia taka, pamoja na kuhamasisha utenganishaji wa taka kulingana na aina zake.

Ili kuimarisha ufuatiliaji, Jiji limejipanga kuajiri vijana waliomaliza mafunzo ya JKT na kuwapatia vyombo vya usafiri kwa ajili ya kusimamia usafi mtaa kwa mtaa.

“Tutakwenda mtaa kwa mtaa. Hatutaki kuona mtu anatupa taka popote anapotaka. Tutakuwa na mfumo wa ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha sheria inatekelezwa ipasavyo,” amesema.




Aidha, amesema barabara zote muhimu za Jiji, maarufu kama Smart Roads, zitasimamiwa kikamilifu ili zibaki safi, zipandwe miti rafiki na salama, na ziendelee kulipamba Jiji.

Amesema biashara katika barabara hizo hazitaruhusiwa bila kibali cha Mkurugenzi wa Jiji, huku wafanyabiashara wakitakiwa kufanya shughuli zao katika maeneo yaliyopangwa. Hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano, kuimarisha usalama na kulinda mandhari ya Jiji.

Akizungumzia mpango huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, alimhakikishia mkuu huyo wa wilaya kuwa uongozi utashirikiana bega kwa bega na wadau mbalimbali wa mazingira kuhakikisha sheria hiyo inatekelezwa kikamilifu katika kata zote 36 za jiji hilo. 

Jitihada hizi za kuimarisha usafi na kupendezesha mazingira zimeongeza kasi kubwa ikizingatiwa kuwa Dar es Salaam inatazamia kuwa mwenyeji mkuu wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), huku wananchi na viongozi wakiendelea na mazoea ya kushiriki shughuli za usafi kila Jumamosi ili kulinda hadhi ya taifa.

No comments