Dkt. Kikwete: Tumeridhishwa na Utekelezaji wa Miradi ya Afya ya JMKF Tabora

 



Rais Mstaafu, Muasisi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF), Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ameeleza kuridhishwa kwake na kukamilika kwa ujenzi wa zahanati na utekelezaji wa Mradi wa Jamii Salama mkoani Tabora.

Akizungumza baada ya ziara yake ya siku nne ya kukagua miradi hiyo katika vijiji vya Gengesita (Wilaya ya Uyui) na Ipembe (Wilaya ya Sikonge), Dkt. Kikwete alibainisha kuwa zahanati hizo zimeshaanza kutoa huduma kwa wananchi.

Aidha aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano wake na JMKF, pamoja na kuishukuru kampuni ya Marekani ya S.C. Johnson & Son kwa kufadhili miradi hiyo iliyolenga kusogeza huduma za afya karibu na wananchi wa maeneo ya pembezoni.

Zahanati hizo zimejengwa kutoa huduma kamili za afya ya msingi, ikiwemo idara ya wagonjwa wa nje, kliniki ya afya ya uzazi na mtoto, wodi ya wazazi, vyoo vya umma, kichomea taka, mashimo ya kondo la nyuma, na nyumba mbili za watumishi ili kusaidia upatikanaji na uwepo wa kudumu wa wataalamu wa afya, hasa wauguzi wakunga, maeneo hayo ya mbali.












Utekelezaji wa miradi hii unatoa suluhu ya kudumu kwa changamoto ya muda mrefu ya umbali mkubwa uliokuwa ukiwakabili wakazi wa vijiji hivyo—vikiwa takribani kilomita 152 kutoka makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Uyui na kilomita 199 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge—hali iliyokuwaikosesha wajawazito, watoto, wazee na wagonjwa huduma za haraka.

Hatua hii ya ujenzi inatokana na mafanikio ya kliniki tembezi zilizoendeshwa na JMKF mwanzoni mwa mwaka 2025 ambapo mamia ya kina mama wajawazito walipatiwa huduma bila malipo. Kutokana na ukubwa wa mahitaji yaliyoshuhudiwa, JMKF iliamua kujenga zahanati hizo ili kuweka msingi wa huduma za kudumu.

Kupitia mafanikio hayo, JMKF imesema itaendelea kushirikiana na Serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa jamii zinazoishi katika maeneo yenye changamoto ya kufikia vituo vya kutolea huduma.

 

No comments