Jeshi la Magereza Laokoa Sh Bilioni 1.9 Baada ya Kujitosheleza kwa Chakula
JESHI la Magereza limefanikiwa kuokoa shilingi bilioni 1.9 ndani ya miezi miwili ya Julai na Agosti 2026 baada ya kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 100 kupitia mavuno ya msimu wa kilimo wa 2025/26.
Mafanikio hayo yalbainika juzi wakati Mkuu wa Jeshi la Magereza, Kamishna Jenerali wa Magereza, Jeremiah Katungu alipofanya kikao kazi kwa njia ya mtandao na wakuu wa magereza wa mikoa katika ukumbi mdogo wa CGP, Msalato jijini Dodoma.
Akisoma ripoti ya mkakati wa kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa na mahabusu, Mkuu wa Kitengo cha Kilimo na Mifugo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Daimu Mmolosha alisema kuwa tangu Julai 2026 jeshi hilo limeacha kununua chakula kutoka nje na sasa linajitegemea kikamilifu.
Kutokana na mafanikio hayo, Katungu alizipongeza taasisi na magereza yaliyofanya vizuri na kufanikiwa kugawa chakula katika vituo vingine nchini, akilitaja Gereza la Kilimo Pawaga, Iringa kuwa limefikia lengo la uzalishaji na kugawa mpunga kwa matumizi ya mwaka mzima katika vituo mbalimbali.
Vilevile, Gereza la Kitete limezalisha na kusambaza mahindi, wakati Gereza la Kalilankulukulu limesambaza mahindi katika magereza makubwa yakiwemo Arusha, Ukonga, Segerea, Keko, Isanga Dodoma, Karanga, Ruanda, Lilungu, Butimba Mwanza, Uyui Tabora na Maweni Tanga. Katungu aliwataka wakuu wa magereza nchini kuendelea kutekeleza mikakati mikuu ya jeshi hilo, ikiwemo kuanzisha viwanda vidogo vya kusimika mitambo ya kuchakata nishati mbadala na kukamilisha mifumo ya mahakama mtandao.
Katika hatua nyingine ya kulinda mazingira na kurahisisha utekelezaji wa majukumu, Mkuu wa Sehemu ya Ujenzi, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Kizito Jacka alisema mashine 61 zimenunuliwa kwa ajili ya kutengeneza mkaa mbadala, huku akibainisha kuwa hadi sasa vituo 15 vimeanza kuzalisha mkaa huo wakati ujenzi wa vibanda vya mitambo ukiendelea katika vituo vilivyosalia.

Post a Comment