Ardhi Clinic yawezesha 308 kupata hati za ardhi
Jumla ya hati 308 za umiliki wa ardhi zimetolewa katika zoezi maalum la "Ardhi Clinic" lililohitimishwa Septemba 11,2026 kata ya Zingiziwa jijini Dar es salaam.
Katika zoezi hilo Mkuu wa wilaya ya Ilala Mhe. Mpogolo, Mstahiki Meya wa Jiji hilo Nurdin Bilal (Shetta) na Mkurugenzi wa Jiji Elihuruma Mabelya walikabidhi hati hizo katika hafla fupi iliyofanyika ofisi za Kata hiyo.
Akizungumza katika utoaji wa hati hizo Mhe. Mpogolo amesema wananchi hao wamesubiri kwa muda mrefu hati hizo hali ambayo ilichangia migogoro ya ardhi katika eneo hilo.
“Mhe. Rais amefanya jambo kubwa sana kutoa maelekezo ya kushuka huku chini kushughulikia migogoro hii ya ardhi, kama sio mheshimiwa Rais watu hawa 308 wangepata wapi hati hizi?" Alihoji.
Kwa upande wake Mstahiki meya wa Halmashauri ya Jiji hilo Nurdin Bilal amemhakikishia Mkuu wa wilaya kuwa watahakikisha zoezi hilo linafanyika kata zote 36 ili kumaliza migogoro ya ardhi katika Halmashauri hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam, Elihuruma Mabelya amesema wajibu wa kutatua changamoto za wananchi hasa suala la migogoro ya ardhi na zoezi hilo litaendelea katika eneo hilo kwa kumuweka afisa ardhi atakayeratibu zoezi hilo.
Katika kliniki hiyo maalum zaidi ya maombi 3, 200 yamepokelewa na tayari hati 308 zimetolewa katika kipindi cha siku 14 huku baadhi ya wananchi wakipongeza hatua hiyo iliyosaidia kupata hati hizo ndani ya muda mfupi.

Post a Comment