MSIGWA ATAKA MAOFISA HABARI WA SERIKALI KUPAMBANA NA UPOTOSHAJI MITANDAONI



Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ameagiza moafisa habari serikalini kutumia nafasi zao kupunguza upotoshaji unaoenea mitandaoni, akieleza kuwa wananchi hususan vijana wanaweza kupotoshwa kama serikali isipotoa taarifa kwa wakati. 

Msigwa alitoa mfano wa ujenzi wa reli akisema badala ya maofisa habari kuishia kuripoti ziara za viongozi kwenye miradi, wanapaswa kuwaeleza wananchi na vijana, fursa zinazoweza kupatikana kutokana na uwekezaji huo. 

“Vijana wangapi leo hii wanawekeza kando kando ya reli wakijiweka tayari kusafirisha bidhaa zao kwenda Dar es Salaam au nje ya nchi ili wanufaike na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali?” alihoji Msigwa. 

Msigwa alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wapya wa serikali walioajiriwa wizarani jijini Dodoma juzi. 

Alisema kazi ya maofisa habari si kuwatangaza viongozi bali kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na muhimu kuhusu kazi zinazofanywa na serikali na fursa zinazotokana na miradi. 

“Hatukusema tuanzishe vitengo vya habari serikalini kwa ajili ya ku-promote (kuwatangaza) viongozi; ni kwa ajili ya ku-promote (kutangaza) kazi za serikali,” alisema Msigwa. 

Aidha, aliwataka maofisa habari watoe taarifa kuhusu fursa za kilimo ikiwemo ruzuku za pembejeo na fursa ya uzalishaji wa parachichi katika Nyanda za Juu Kusini. 

Msigwa alisema kurasa za taasisi nyingi za serikali zimekuwa zikijaa picha na taarifa za viongozi, hali inayozifanya zisiwe na mvuto kwa wananchi. 

“Tusipojiangalia, na sisi tutaacha kazi yetu ya kitaaluma ya kuwa maofisa habari, tukaanza kufanya kazi ya kuwa ‘chawa’. Hatupaswi kuwa ‘chawa’ wa viongozi,” alisema. 

Msigwa aliwataka maofisa habari hao wapya wazingatie utendaji, uaminifu, bidii na sheria za utumishi wa umma akisisitiza mafanikio katika utumishi yanapaswa kujengwa kupitia utendaji kazi wenye matokeo.

 Alisema watumishi wanaolalamika kila mara, kuanzisha fitina na migogoro kazini au kuwachonganisha wenzao kwa viongozi hawatafanikiwa na kuwataka watumie muda wao kujifunza na kufanya kazi kwa bidii.


No comments