AI itumike kuhifadhi utamaduni Tanzania
UHIFADHI wa utamaduni umeingia katika hatua mpya ya mageuzi kupitia Akili Unde (AI) katika ulimwengu ambao teknolojia inakua kwa kasi.
AI sasa imekuwa zaidi ya programu ya kompyuta na ni daraja kati ya kumbukumbu zinazofifia za mababu na uhalisia wa kidijiti wa kizazi cha sasa.
Matumizi ya teknolojia hiyo katika nyanja ya utamaduni yanakuja na mlinganyo wa kijasiri; uwezo wa kujenga upya kile kilichopotea au uwezo wa kubomoa kabisa msingi wa ukweli wa kihistoria ikiwa mwanadamu ataruhusu ubongo wake kulala. Matumizi ya AI katika utamaduni yanaweza kufananishwa na kisu ambacho kinatumika jikoni kukatia nyanya kuandaa mlo mtamu wa familia, lakini kisu hicho hicho kinaweza kutumika kama silaha.
Katika muktadha wa utamaduni, AI inaweza NUKUU kutumika kusafisha sauti za nyimbo za asili, kuchora upya picha za mashujaa wetu wa kale na kuandika upya hadithi zetu zilizokuwa zimesahaulika lakini upande wa pili, inaweza kupotosha.
AI haipaswi kutumiwa kama mbadala wa ubongo wa mwanadamu ni lazima itumike kama zana ya kufanyia kazi kwani hatari inayotukabili ni kuwa wazembe wa kufikiri na kuacha kila kitu mikononi mwa teknolojia.
Ikiwa utaruhusu AI ikuwazie, itakutengenezea utamaduni usio na uhalisia, hivyo mwanadamu lazima abaki kuwa ndiye mwenye kumbukumbu, hisia na uchungu wa asili yake.
Tukishindwa kuwaza wenyewe, tutashindwa kutoa maelekezo sahihi na matokeo yake yatakuwa ni picha au sauti zinazofanana na utamaduni kwa nje. Ukisimulia vizuri kumbukumbu yako ya kale ukaelezea kwa undani mavazi, mazingira, hisia na hali ya hewa ya wakati huo, AI ina uwezo wa kuchora picha ya tukio hilo kwa usahihi wa hali ya juu.
Nchi nyingi duniani zimeanza kutumia AI kama sehemu ya uvumbuzi wa kitaifa kuhakikisha kuwa utamaduni wao haufi kwani utamaduni usiobadilika mara nyingi hufa. Siri ya kufanikiwa kutumia AI bila kupotosha ni lazima kuwe na mlinzi wa maudhui ambaye anahakikisha kinachozalishwa na AI kinabaki kuwa na ukweli wa kihistoria.
Hapa, fikira za ndani za mwanadamu ndizo zinazotoa uhai kwa mashine na AI inakuwa kama brashi ya mchoraji na unaweza kuelezea kila kona ya hadithi unayotaka mpaka ikapatikana taswira kamili inayogusa hisia.
Katika sekta ya muziki, hasa wa asili AI inakuja kama mkombozi wa kiuchumi na kiufundi kwani kurekodi wimbo mmoja wenye viwango vya kimataifa unahitaji si chini ya Sh 300,000 kwa ajili ya studio pekee. Lakini kwa kutumia AI msanii anaweza kujirekodi kwenye kompyuta yake na kupitia zana za AI, akaielekeza mashine kuchanganya sauti, kuondoa kelele za nyuma na kupandisha ubora wa sauti kufikia kiwango cha studio ya gharama.
Hiyo inamaanisha kuwa utamaduni wa sifa, nyimbo za mavuno, na mdundiko vinaweza kurekodiwa na kuhifadhiwa katika ubora ambao kizazi cha sasa kitaupenda na kuufurahia kwenye majukwaa ya kidijiti kama Spotify au YouTube bila kupoteza asili yake. Ikiwa utabweteka na kuiacha AI iamue kila kitu, utapata picha za mashujaa wakiwa wamevaa mavazi ya kigeni au nyimbo zao zikiwa na mahadhi yasiyolingana na asili yako. Uzembe wa kifikira utatupelekea kuwa na kizazi ambacho hakiwezi kuhadithia hadithi hata moja bila kuomba msaada wa AI. Hapo ndipo ubomoaji wa utamaduni utakapoanzia.

Post a Comment