Tanzania Yaahidi Ushirikiano Ujenzi wa Mifumo Imara ya Afya
Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana kwa karibu na WHO, taasisi za kikanda, washirika wa maendeleo na nchi wanachama katika kujenga mifumo ya afya imara, yenye usawa na inayomlenga mwananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi, Agosti 25, 2026 kwenye Mkutano wa 76 wa Kamati ya Kanda ya Afrika ya Shirika la Afya Duniani (WHO-AFRO), unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Aidha alisema Tanzania inaunga mkono juhudi za kuimarisha Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia maboresho ya Muundo wa Mfumo wa Afya Duniani (Global Health Architecture), na kusisitiza umuhimu wa WHO kuendelea kutekeleza jukumu lake la msingi kama mamlaka ya kiufundi ya afya duniani.
"Tanzania inaipongeza WHO kwa kuratibu ushiriki wa Kanda ya Afrika kwenye utekelezaji wa marekebisho ya Kanuni za Kimataifa za Afya (International Health Regulations – IHR 2024) pamoja na kukamilishwa kwa viambatisho vyake katika Mkataba wa WHO," amesema Dkt. Samizi.
Aidha, Dkt. Samizi amesema Tanzania inatambua mchango wa Shirika la Afya Duniani(WHO )katika kutoa msaada wa kiufundi ili kuimarisha mifumo ya afya, kuboresha ufuatiliaji wa magonjwa, kukabiliana na milipuko, kuendeleza huduma jumuishi za afya kwa wote pamoja na kuboresha afya ya mama na mtoto pamoja na vijana.

Post a Comment