TUMIENI MICHEZO KUDUMISHA AMANI NA UPENDO KATIKA JAMII



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ,SACP, Marco G. Chilya, amewataka Maafisa, Wakaguzi, Askari wa vyeo mbalimbali pamoja na wananchi kutumia michezo kama jukwaa muhimu la kudumisha amani, upendo, mshikamano na kujenga mahusiano mazuri kati ya Jeshi la Polisi na jamii. 

Wito huo umetolewa katika Uwanja wa Majimaji, Manispaa ya Songea, wakati wa Bonanza la Polisi Jamii Cup lililoandaliwa kuelekea maadhimisho ya Miaka 20 ya Polisi Jamii, likihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, riadha za mita 100 na 200 kwa wanawake na wanaume, pamoja na mchezo wa kuvuta kamba ambapo polisi walishindana na timu kutoka katika jamii.

Mashindano hayo yaliyoshirikisha wananchi na askari katika nyanja mbalimbali za michezo yametumika kuimarisha uhusiano, ushirikiano na kupeana elimu kuhusu umuhimu wa kushirikiana katika kudhibiti uhalifu katika jamii.






Katika mchezo wa mpira wa miguu kati ya timu za Shule za Sekondari Songea Boys na Emmanuel Nchimbi, timu ya Emmanuel Nchimbi iliibuka mshindi kwa bao 1-0. 

Katika fainali ya mpira wa miguu, timu ya Polisi Wilaya ya Nyasa ilikutana na timu ya FFU Ruvuma, ambapo FFU Ruvuma iliibuka mshindi kwa mikwaju ya penalti na kutwaa Kombe la mashindano hayo, huku washindi katika michezo mbalimbali wakikabidhiwa zawadi zilizojumuisha medali, mipira na kombe kama sehemu ya kutambua juhudi na ushiriki wao katika kufanikisha bonanza hilo.












Akizungumza wakati wa hafla hiyo, SACP Chilya amesisitiza kuwa michezo si kwa ajili ya burudani pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kuwakutanisha watu, kujenga urafiki, kuimarisha mshikamano na kutoa fursa ya kuelimishana kuhusu madhara ya kujihusisha na vitendo vya uhalifu huku akiongeza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Polisi na wananchi ni msingi thabiti katika kuzuia na kudhibiti uhalifu pamoja na kujenga jamii salama na yenye amani wakati wote.

Aidha, SACP Chilya amewapongeza Maafisa, Wakaguzi, askari wa vyeo mbalimbali pamoja na wananchi wote walioshiriki kwa wingi katika bonanza hilo na kuwataka kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Jeshi la Polisi na wakazi wa Mkoa wa Ruvuma kupitia michezo na shughuli nyingine za kijamii.

No comments