HALMASHAURI YA JIJI DAR ES SALAAM YANG’ARA NANE NANE, YABEBEA VIKOMBE VYA UBINGWA



HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam imeibuka kidedea katika Maonesho ya Wakulima Nane Nane Kanda ya Mashariki yaliyofanyika Morogoro, baada ya kutwaa vikombe vya ushindi katika nafasi ya kwanza kwa Mkoa wa Dar es Salaam na pia kuibuka mshindi wa jumla wa Kanda ya Mashariki mwaka 2026.

Katika maonesho hayo yaliyoshirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, biashara na teknolojia, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Ilala imeonyesha ubunifu na uwezo mkubwa katika kuwasilisha shughuli na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotekelezwa katika Jiji hilo.

Ushindi huo unaifanya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuwa mshindi wa kwanza kwa Mkoa wa Dar es Salaam, huku ikitwaa pia ubingwa wa jumla wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki kwa mwaka 2026.

Akizungumza wakati wa kufunga Maonesho hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu, Watu Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema lengo la Serikali kupitia Maonesho ya Wakulima Nane Nane ni kuwawezesha wakulima wadogo na wakubwa kiuchumi kwa kuwapatia fursa za kujifunza, kuonyesha bidhaa zao, kupata masoko na kuunganishwa na teknolojia pamoja na mitaji.

Profesa Kabudi amesema maonesho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wakulima, wafanyabiashara, wawekezaji, wataalamu na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo na hivyo kuchochea maendeleo ya sekta hiyo.

Amewapongeza wadau wote walioshiriki katika maandalizi na utekelezaji wa maonesho hayo, akiwemo Kamati ya Maandalizi, kwa mchango wao katika kuhakikisha maonesho hayo yanafanikiwa na kuvutia idadi kubwa ya wananchi.

Aidha, amewapongeza washiriki wote, wakiwemo waliofanikiwa kupata tuzo na washindi katika maeneo mbalimbali, pamoja na wale ambao hawakupata ushindi, akisisitiza kuwa ushiriki wao ni sehemu muhimu ya kujifunza na kuboresha kwa maonesho yajayo.

«“Serikali itaendelea kuhamasisha programu mbalimbali pamoja na mashamba darasa, kwa sababu maendeleo ya kilimo yanahitaji ushirikiano wa sekta zote,” amesema Profesa Kabudi.»

Amesema Serikali pia inaendelea kusimamia utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, ikiwemo kuhakikisha Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki yanaendelea kuwa endelevu na yanatumia ubunifu na teknolojia katika kuimarisha sekta ya kilimo.





Katika hatua nyingine, Profesa Kabudi amezitaka mikoa yote kuhakikisha elimu, teknolojia na mbinu bora za kilimo zinazoonyeshwa katika maonesho hayo zinawafikia wananchi moja kwa moja kupitia mashamba darasa, ili wakulima waweze kujifunza kwa vitendo na kutumia maarifa hayo katika kuongeza uzalishaji na kipato.

Aidha, amewahimiza wananchi wanaofanya kazi katika sekta binafsi kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kupata fursa ya huduma muhimu, ikiwemo bima ya afya na mafao ya pensheni baada ya kustaafu.

Amesema Serikali inaendelea kuhamasisha Watanzania wote, hususan wale walio katika sekta binafsi, kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii, ikiwemo NSSF, ili kujenga uhakika wa maisha yao ya baadaye.

Ushindi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki unaendelea kuonyesha jitihada za Jiji katika kuibua, kuendeleza na kutangaza fursa za kiuchumi zinazopatikana katika maeneo yake, hususan katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, biashara na ubunifu.

No comments