Goat Races ndani ya viwanja vya Posta, Septemba 19



Jumla ya mbuzi 80 wanatarajiwa kushiriki katika mbio za kihistoria za mbuzi zinazojulikana kama The Goat Races ambazo zimelenga kukusanya Shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuchangia huduma mbalimbali za jamii.

Aidha mbio hizo mwaka huu zimepangwa kufanyika Septemba 19 katika viwanja vya Posta Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Rais wa Rotary Club ya Dar es Salaam Oysterbay, Paul Muhato, amesema kuwa fedha hizo zitaelekezwa katika kutoa ufadhili wa masomo kwa watu waliopo na wanaojiunga na vyuo vikuu na vyuo vya kati, sambamba na kuboresha masuala ya afya.

Katika mbio hizo zilizohamishwa kutoka viwanja vya zamani vya Green Oysterbay kutokana na maandalizi ya michuano ya Afcon 2027 na kupelekwa viwanja vya Posta, klabu hiyo imejipanga kuvunja rekodi ya mwaka jana ambapo walifanikiwa kukusanya Sh milioni 160.

“Goat Races ni tukio la kufurahia siku nzuri pamoja huku tukifanya jambo lenye maana kwa jamii. Mwaka huu tunakuja kwa ukubwa zaidi na tumeandaa Safari Adventure yenye burudani na msisimko kwa familia nzima, yote ikiwa ni kwa ajili ya kusaidia jambo jema. Tunaualika umma mzima kuungana nasi.”

Aidha Muhato alimtangaza rasmi mdhamini mkuu wa tukio hilo kuwa ni Vodacom Tanzania itakayochangia Sh milioni 150 pamoja na kugharamia uandaji wa tamasha hilo ambalo linatarajiwa kuhudhuriwa na watu 5,000 huku muda wake ukiongezwa hadi saa nne usiku kuanzia saa sita mchana.



Akizungumza wakati wa kutangazwa rasmi kwa udhamini huo, Bwana Joseph Sayi, Mkuu wa Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Tanzania, alisema kampuni hiyo inajivunia kuendelea kuunga mkono mpango ambao tayari umeonyesha matokeo halisi katika jamii.

“Ushirikiano wetu na Rotary Club of Dar es Salaam Oyster Bay, ambao sasa umefikia mwaka wa nne, tayari umesaidia kuboresha miundombinu ya shule na kutoa ufadhili wa masomo kwa zaidi ya wanafunzi 350 wenye uhitaji katika taasisi za elimu ya juu na mafunzo ya ufundi stadi.

“ Mwaka huu, tunaendeleza mafanikio hayo kwa kuboresha zaidi mazingira ya kujifunzia pamoja na huduma za maji, usafi na usafi wa mazingira. Tunazialika taasisi nyingine kuungana nasi ili kwa pamoja tuweze kuleta matokeo makubwa zaidi katika jamii.” Alisema Sayi

 Aliongeza kuwa kurejea kwa Vodacom kama Mdhamini Mkuu kunaonyesha imani ya kampuni hiyo katika matokeo yanayopatikana kupitia mpango huu, pamoja na uwezo wa Rotary kuendelea kuandaa moja ya matukio makubwa na yanayosubiriwa kwa hamu zaidi ya kuchangisha fedha kwa ajili ya jamii jijini Dar es Salaam.

Mratibu wa Mbio za Mbuzi, Bi. Rashida Nas, aliukaribisha ushirikiano unaoendelea kati ya Vodacom Tanzania na Rotary, pamoja na mchango mkubwa wa wadhamini na washirika wengine wanaorejea mwaka huu.

“Tunafurahi sana kuwa na Vodacom Tanzania kama mdhamini wetu kwa mara ya nne, na tunawashukuru kwa kuendelea kutuamini, pamoja na wadhamini na washirika wetu wote. Tukiwa katika eneo jipya na kubwa zaidi, ambapo watoa huduma mbalimbali wa vyakula na vinywaji pamoja na burudani watashiriki nasi siku nzima, Goat Races 2026 itakuwa ni sherehe inayoonyesha nguvu ya ushirikiano katika kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu nchini Tanzania.”

Akielezea taratibu za ushiriki na viingilio, Muhato amesema kuwa mtu au taasisi inayotaka kununua mbuzi wa mashindano inawapata kwa Shilingi laki saba, dau ambalo ni sawa na kukata tiketi nne za VIP kwa bei nafuu.

Tiketi moja ya VIP kwa sasa inauzwa kwa Sh laki mbili na itapanda na kuwa Sh 230,000 mwezi ujao kabla ya kuuzwa Sh 250,000 getini, wakati tiketi za kawaida zikiwa ni Sh elfu 30, watoto wenye umri wa miaka 12 wakilipia elfu kumi, na watoto chini ya miaka mitano wakiruhusiwa bure chini ya kauli mbiu ya Safari Adventure.



Katika ufafanuzi wake kuhusu msaada wa elimu, Muhato alibainisha kuwa hadi kufikia mwaka huu wa 2026, jumla ya watu 350 wamefadhiliwa kupitia mapato ya mbio hizo, ambapo kwa mwaka jana pekee wa 2025 waliwafadhili watoto 100 katika vyuo mbalimbali, wanafunzi 30 wa vyuo vya ufundi na amali, pamoja na watu sita waliopata ufadhili katika vyuo vya usafiri wa anga.

Muhato alisisitiza kuwa ufadhili huo hutolewa kwa wenye mahitaji kupitia vigezo maalumu kama vile alama bora za darasani, ukosekanaji wa ufadhili mwingine, na kupata nafasi ya chuo.

Mbali na burudani, chakula, na msisitizo wa mavazi ya asili ya safari, tukio hilo litatoa zawadi mbalimbali kwa washindi wa mbio na wale watakaovaa vizuri zaidi.

Wakati huo huo, Muhato alibainisha kuwa Rotary ya Oysterbay ipo katika hatua za mwisho za kufanya mpango wa kutiliana saini mikataba ya ushirikiano na wizara zinazohusika na elimu na afya ili kuendeleza na kurahisisha juhudi zao za kuwezesha upatikanaji wa huduma bora nchini, huku akiwasihi wananchi kutembelea tovuti ya goatraces.tz kujipatia tiketi mapema.

No comments