Tanzania na OACPS Zaimarisha Ushirikiano wa Kimkakati Arusha
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amekutana na kufanya mazungumzo jijini Arusha na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS), Mhe. Moussa Saleh Batraki.
Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais alimhakikishia dhamira thabiti ya Tanzania ya kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa taasisi hiyo ili kuleta mageuzi na tija kwa nchi wanachama.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais alimpongeza Katibu Mkuu huyo kwa jitihada zake za kutekeleza ajenda ya mageuzi inayolenga kuongeza uadilifu na kupunguza utegemezi ili kufanya jumuiya hiyo kuwa na nguvu zaidi katika uwanja wa kimataifa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa OACPS, Mhe. Moussa Saleh Batraki, aliweka wazi vipaumbele vya taasisi hiyo vinavyojumuisha kuimarisha biashara na mtangamano miongoni mwa nchi wanachama, pamoja na kujenga uhimilivu thabiti wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aliongeza kuwa jumuiya hiyo imeweka mkazo mkubwa katika uwekezaji wa TEHAMA, hususan teknolojia za kidijitali, akili unde, na ulinzi wa takwimu, sambamba na kuinua uchumi wa wanawake na kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya nchi zinazoendelea.
Mkutano huo muhimu ulihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali akiwemo Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas Nyamanga, pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Ellen Maduhu.

Post a Comment