MAPATO YA NDANI KUBEBA BAJETI YA TRILIONI 62 YA 2026/2027
Serikali imekamilisha mchakato wa kupokea na kuchambua maoni 727 kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu maboresho ya mfumo wa kodi na tozo kwa mwaka wa fedha 2026/27, huku ikitarajia kutumia jumla ya shilingi trilioni 62.3 katika mwaka huo wa fedha.Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema maoni hayo yalitolewa na taasisi za Serikali, sekta binafsi, kampuni na wananchi, yakihusu masuala ya kikodi, kisheria na kiutawala.
Amesema maoni hayo yalichambuliwa na kikosi kazi kilichojumuisha wadau kutoka sekta za umma na binafsi, ambapo mapendekezo 125 yalikubaliwa kama yalivyo, 121 yakafanyiwa marekebisho kabla ya kupitishwa, huku 295 yakikataliwa baada ya kufanyiwa tathmini ya kina.
Aidha, amesema mapendekezo 107 yamepelekwa katika wizara na taasisi husika kwa ajili ya ufafanuzi zaidi, 47 hayakufanyiwa uamuzi kutokana na upungufu wa taarifa, na 32 tayari yapo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Balozi Omar amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuboresha mazingira ya kodi kwa maendeleo ya taifa.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema Serikali inatarajia kutumia shilingi trilioni 62.3 katika mwaka wa fedha 2026/27, kwa mujibu wa mwelekeo wa bajeti uliowasilishwa bungeni Januari mwaka huu.
Ameeleza kuwa sehemu kubwa ya bajeti hiyo itagharamiwa na mapato ya ndani yanayokadiriwa kufikia shilingi trilioni 46.8, jambo linaloonyesha kuendelea kuimarika kwa uwezo wa nchi kugharamia maendeleo yake kupitia rasilimali za ndani.
Kwa mujibu wa Waziri Omar, mchanganuo wa kina wa mapato na matumizi ya Serikali utawasilishwa rasmi bungeni Juni 11, 2026 wakati wa uwasilishaji wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Bajeti hiyo itakuwa ya kwanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na ni kubwa zaidi ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2025/26 iliyokuwa na thamani ya shilingi trilioni 56.4.

Post a Comment