Jinsi Serikali Inavyomwaga Mitaji, Kupiga Jeki Ajira za Vijana na Kuzika Vurugu
KATIKA mazingira ya sasa ya kiuchumi duniani, silaha kubwa ya kupambana na ukosefu wa ajira kwa vijana siyo maneno matupu ya kisiasa au ahadi za majukwaani, bali ni kuweka mifumo thabiti ya kifedha inayochochea uzalishaji.
Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya taasisi hiyo, imeonesha wazi taswira ya namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyopigana usiku na mchana kufungua milango ya kiuchumi kwa ajili ya vijana wa Kitanzania, kupitia mageuzi makubwa ya sekta ya fedha na kibenki.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, alifichua takwimu muhimu zinazothibitisha kuwa Tanzania sasa imekuwa chemchemi ya fursa. Moja ya takwimu hizo ni ongezeko kubwa la mikopo kwa sekta binafsi, ambayo imepaa kutoka asilimia 6.6 ya Pato la Taifa mwaka 1994 hadi kufikia takribani asilimia 16 mwaka 2025.
Wakati wachumi wakiangalia takwimu hizi kama ushindi wa sera za kifedha, kwa kijana aliyepo mtaani au anayemaliza chuo, hii ni habari njema ya upatikanaji wa ajira.
Sekta binafsi ndiyo mwajiri mkuu nchini. Ongezeko hili la mikopo maana yake ni kwamba mabenki yameaminiana na Serikali imetengeneza mazingira salama, kiasi kwamba wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda, makampuni ya kilimo, na wajasiriamali sasa wanapata mitaji kwa urahisi zaidi kuliko wakati wowote katika historia ya nchi hii.
Kiwanda kinapopata mkopo, kinapanua uzalishaji na kuajiri wahandisi vijana, madereva, na wahasibu. Kampuni ya ujenzi inapopata mkopo, inahitaji vijana wa kufanya kazi za ujenzi. Hata kijana mjasiriamali anayetaka kuanzisha biashara yake, sasa anazungukwa na mazingira ambapo huduma rasmi za kifedha zimefikiwa kwa asilimia 89, shukrani kwa ujumuishi wa kifedha na mifumo ya kidijitali.
Zaidi ya hayo, Gavana Tutuba alibainisha kuwa viwango vya mikopo chechefu (mikopo inayoshindikana kulipwa) vimeshuka kwa kasi ya ajabu hadi asilimia 2.9 mwezi Februari 2026, ikiwa ni chini kabisa ya kiwango cha hatari cha asilimia tano. Hii ina maana biashara za Kitanzania zinazokopeshwa zinastawi, zinatengeneza faida, na zina uwezo wa kudumu—jambo linalohakikishia usalama wa ajira kwa vijana walioajiriwa.
Mkakati huu wa serikali wa kuimarisha sekta binafsi na kukuza uchumi kwa wastani wa asilimia 6.2 (zaidi ya wastani wa Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao ni asilimia 4.4), una dhumuni lingine kubwa: Kulinda nguvu kazi ya Taifa dhidi ya uharibifu.
Kijana mwenye ajira rasmi, kijana mwenye duka linalokua, au kijana anayesubiri kuvuna bustani yake ya mboga iliyofadhiliwa na mkopo wa benki, hana muda wa kwenda barabarani kufanya maandamano ya kuchoma shule, vyuo, au miundombinu. Anaelewa kuwa uharibifu wa nchi ni uharibifu wa biashara yake, ajira yake, na kesho yake.
Serikali, kupitia BoT, imeamua kumkomboa kijana kiuchumi ili asishawishike kwa vipande vichache vya fedha kutoka kwa wanasiasa wenye nia ovu wanaotaka kuwatumia vijana kama ngao ya kufanyia fujo.
Inapofikisha akiba ya fedha za kigeni kutosheleza miezi 4.8 na kununua tani 27.5 za dhahabu zenye thamani ya Sh trilioni 10, serikali inajenga ukuta imara wa kulinda uchumi usiyoyoma, ili biashara za vijana zisiathirike na mfumuko wa bei.
Mageuzi haya ya kiuchumi ni ujumbe tosha kwa vijana wote wa Kitanzania: Serikali yenu inawapigania kwa vitendo, siyo kwa maneno. Imeweka fedha kwenye mabenki, imeshusha riba, imedhibiti mfumuko wa bei hadi asilimia 3.5, na imefungua milango ya sekta binafsi ili mkaajiriwe na mkaajiri wengine.
Wakati mabenki 42 nchini yakishindana kutoa mikopo kwa sekta binafsi, wajibu wa vijana ni kuchamkia fursa hizi kwa kuandika maandiko mazuri ya biashara, kujiunga kwenye vikundi, na kujiajiri.
Ni marufuku kukubali kupoteza muda mtaani kusikiliza mbinu za kuchoma moto nchi au kuharibu miundombinu ya elimu. Ukishachoma chuo au shule, unakuwa umejifungia mlango wako mwenyewe wa kutengeneza kesho iliyo bora. Serikali imeshatandika mkeka wa kiuchumi; kazi ya vijana ni kukanyaga kwa ujasiri na kujenga maisha yao.

Post a Comment